Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Jakaya Kikwete amemsifu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea wa nafasi ya Urais wa Tanzania kama Kiongozi mwenye maono, akishughulikia kikamilifu changamoto za wananchi, akimtakia kheri na ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu Mjini Kibaha Mkoani Pwani leo Jumapili Septemba 28, 2025, Dkt. Kikwete amemuahidi Dkt. Samia kura za kishindo kutoka Mkoani Pwani, akimpongeza pia kwa namna ambavyo amefanikiwa kuzikabili changamoto za wananchi kwa mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa serikali ya awamu ya sita.
"Umezikabili kwa mafanikio changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkoa huu, tena umezikabili kwa ufanisi, umakini na ujasiri mkubwa. Umetutendea mema na mazuri mengi na ni wajibu wetu sasa kukulipa mema. Tutakulipa kwa mema uliyotutendea. Kama bunge linalomalizika sasa wabunge wote ni wa CCM na litakalokuja Wabunge wote kutoka Pwani watatokana na Chama Chs Mapinduzi na kwa nchi nzima naamini itakuwa hivyo." Amesema Dkt. Kikwete.
Kiongozi huyo mstaafu kadhalika amemtaja Dkt. Samia kama Mama mwema, akisema Tanzania imeendelea kuwa na umoja na mshikamano katika kipindi chake cha serikali ya awamu ya sita, akiwasisitiza wananchi wa Pwani kutofanya makosa ya kuchanganya Viongozi kutoka vyama vingine na badala yake wachague Madiwani na Wabunge wanaotokana na Chama tawala, Chama Cha Mapinduzi.

Post A Comment: