Na Mwandishi Wetu, Mbeya


MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amemhakikishia Usalama wakati wote wa huduma za kiroho atakazofanya Jijini Mbeya, mhubiri wa Kimataifa kutoka nchini Kenya Pastor Ezekiel.


Sambamba na kumhakikishi Usalama, DC Itunda alipongeza ujio wa Mhubiri huyo wa Injili wa Kimataifa kutoka nchini Kenya, ambaye atafanya mahubiri yake Jijini Mbeya.


Pastor Ezekiel atamwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uchaguzi Mkuu ujao pamoja na amani ya Taifa, hatua ambayo DC Itunda ameieleza kuwa ni ya baraka kubwa kwa nchi.

Akizungumza baada ya kupokea wageni hao, DC Itunda alisema ujio wa mhubiri huyo ni ishara ya upendo na mshikamano wa Kikristo unaovuka mipaka ya mataifa hayo jirani.


 Aliongeza kuwa maombi kwa Taifa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu ni muhimu kwa ajili ya kudumisha mshikamano na mshikamanifu wa Watanzania wote bila kujali imani zao.


Katika hotuba yake, Pastor Ezekiel aliwahimiza waumini na viongozi wa dini kuendelea kusali kwa ajili ya amani, mshikamano na maendeleo ya Taifa.

Aidha, Pastor Ezekiel atakuwa na mkutano mkubwa wa kiroho jijini Mbeya kuanzia Septemba 24 hadi 28, 2025, ambapo maelfu ya waumini kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki. 


Mkutano huo unatarajiwa kuleta faraja ya kiroho kwa washiriki na kuchangia ustawi wa kijamii kwa jamii ya Mbeya na Tanzania kwa ujumla.

DC Itunda aliwaomba wananchi wa Mbeya kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mkutano huo wa kiroho, akibainisha kuwa mbali na kupata baraka, wananchi pia watakuwa sehemu ya historia ya kipekee ya kuombea Taifa kuelekea uchaguzi mkuu. 


Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuthamini na kushirikiana na viongozi wa dini katika kulinda amani na mshikamano wa Watanzania.

Mwisho

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: