Na Mwandishi Wetu, Muheza

MGOMBEA ubunge Jimbo la Muheza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA amesema katika miaka mitano ijayo atahakikisha anaongeza minara ya simu ili Jimbo la Muheza liweze kuwa na mawasiliano katika maeneo ambayo yana changamoto hiyo.



Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Kwezitu tarafa ya Amani, MwanaFA alikiri kwamba yapo maeneo katika Jimbo hilo, yana changamoto ya ukosefu wa mawasiliano.



"Katika miaka mitano ijayo tutaimarisha mawasiliano ya simu...Moja ya mambo yanayonisikitisha ni kufika baadhi ya maeneo kwenye Jimbo la Muheza ikawa simu haiwezi kushika mawasiliano, huwezi kupigiwa simu," alisema na kuongeza,

"Tunachotaka kufanya ni kuhakikisha tunaongeza minara ya simu ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa mawasiliano kwa wananchi wetu,".



MwanaFA ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2020-2025 Jimbo hilo lilipata minara Saba ambayo kutokana na jiografia ya Jimbo hilo, bado haijakidhi mahitaji ya mawasiliano katika maeneo mengi kutokana na hali hiyo.

Hivyo, alisema anakwenda kuzifanyia kazi kuhakikisha minara ya simu inaongezeka na hali ya mawasiliano inazidi kuimarika katika Jimbo hilo.



"Sitaki kuahidi mambo mengi na nikashindwa kuyatekeleza lakini niwahakikishie jambo moja changamoto zote za kata ya Kwezitu, Jimbo la Muheza kwangu ni kipaumbele...Miaka mitano hii nimejua kona zote za kutatua changamoto zilizopo katika Jimbo letu," alisema.




Aliwaomba wananchi wa Kwezitu kufanya kazi mbili ambazo ni kwenda kupiga kura Oktoba 29 na kuwachagua wagombea wa CCM ili waweze kumalizia kazi ambazo wamezifanya katika miaka mitano iliyopita.



Alisema wananchi wa Kwezitu wanakila sababu za kumchagua Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwakuwa ameleta fedha nyingi katika kata hiyo na Jimbo zima la Muheza.




Rais ameleta fedha nyingi katika miradi ya afya, elimu, maji, barabara na miradi mingine hivyo anastahili kupigiwa kura nyingi katika Jimbo letu.

"Nichagueni na Mimi miaka mitano hii nimeisema wilaya hii, hatuwezi kusema matatizo yetu yote tumeyamaliza bali dhamira yetu ni ya dhati kwakuwa kila sekta tumeigusa," alisema na kuwaomba wananchi wa kata hiyo kumchagua Mch. John Mzalia awe diwani wa kata hiyo.



Akiomba kura kwa wananchi wa kata hiyo Mgombea udiwani Mch Mzalia alisema kuwa kata hiyo imepata miradi mingi kuliko wakati wowote ule ikiwemo miradi ya Elimu, afya, barabara na huduma za jamii.




"Tumepata mradi wa Boost ambao shule yetu ya Kwezitu imekuwa nzuri mno hadi watoto wetu wanasoma kwenye shule ya vioo wakati mwingine wanachungulia kwenye madirisha hayo kama watoto wa Kihindi," alisema na kuwaomba wananchi hao wawachague wagombea wa CCM.




Katibu wa CCM wilaya ya Muheza Simon Leng'ese amewataka viongozi wa CCM wa ngazi zote za kata hiyo kuhakikisha wanatoka na kwenda kwa wananchi kuomba kura za wagombea wa CCM ili kukifanya chama hicho wagombea wake kupata kura za kishindo.



"Viongozi wa kata, matawi, mashina, mabalozi mtoke kwenda kuomba kura kwa wananchi katika maeneo yenu, haya ni maagizo nawapa mwende kukifanya chama chetu na wagombea wetu waweze kupata kura nyingi," alisema Leng'ese.




Meneja wa kampeni wa mgombea wa Jimbo la Muheza Aziza Mshakang'oto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM wilaya ya Muheza (UVCCM), amewataka wananchi wa kata ya Kwezitu wasifanye makosa kwa kuwachagua wagombea wa upinzani kwakuwa hawana jipya.




Alisema CCM imekuja na ilani ambayo kwa wilaya ya Muheza imekuwa na miradi mingi ya maendeleo katika Jimbo hilo hivyo wasifanye makosa katika uchaguzi huo.

Mwisho
Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: