Na Denis , Chambi, Tanga.
WAFANYABIASHARA wanaofanya shughuli zao katika masoko ya Mgandini , Makorora, Mlango wa Chuma na Uzunguni yaliyopo katika halmashauri ya jiji la Tanga wametajwa kuwa moja wapo ya wadau wa kubwa wa maendeleo ambao wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa pato la Mkoa wa huo na kuufanya kushika nafasi ya sita katika mikoa yote iliyopo hapa nchini.
Akizungumza katika Hafla ya kumkabidhi mkandarasi mradi wa ujenzi wa Soko la Makorora, ujenzi wa soko la kisasa la Samaki Deep Sea pamoja na uboreshaji wa fukwe za Raskazone mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt.Batilda Buriani amesema kuwa Mkoa huo katika takwimu za mwaka 2024 kwenye ukusanyaji wa mapato kitaifa umefanikiwa kukusanya zaidi shilingi Bilioni 9.5 fedha hizo zikichagizwa zaidi na Bandari ya Tanga pamoja na wafanyabiashara wa masokoni ambapo bidhaa nyingi zimekuwa zikitoka kwenda mikoa ya jirani ikiwemo Pemba sambamba visiwa vya Comoro na maeneo mengine.
"Jiji la Tanga ni jiji la sita kwa ukusanyaji wa mapato na Bandari yetu imetujengea heshima kubwa, wafanyabiashara wa masoko yetu ya Tanga ikiwemo soko la Mgandini ambalo kuna biashara kubwa inafanyika bidhaa zinakwenda nje ya mkoa ikiwemo Pemba, Comoro, Mombasa na maeneo mengine mapato haya ya Mkoa wetu wa Tanga ambayo yanachangia ukuwaji wa pato la Taifa ni jitihada zenu wafanyabiashara ni lazima tujivunie kwa sababu ni jitihada ambazo zinatokana na uwekezaji unafanywa na Serikali" amesema Dkt. Buriani.
Aidha Dkt. Burian amemtaka Makandari anayetekeleza miradi hiyo ni lazima kuhakikisha anazingatia ubora wa miundombinu ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira safi na salama hatua ambayo itawasaidia kujipatia kipato na kuendelea kuchangia ukuwaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja na kwa Taifa.
"Mradi huu kama ukikamilishwa vizuri bila shaka itaimarisha sana uwezo wa Halmashauri yetu katika kuhudumia wananchi ya kuwa na masoko mazuri ambayo hayana kero ndugu zetu wataendelea kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa sana tunatamani Tanga ifike katika 3 bora ya mikoa inayokusanya mapato mengi Tanzania nafikiri tutaweza"
Amesema uchumi wa Tanga unaendelea kukua siku hadi siku kutokana na upatikanaji wa mafuta ambapo Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayoongoza hapa nchini katika biashara ya mafuta ambapo kupitia kampuni ya GBP kwa siku zaidi ya magari mia mbili yanajaza na kusafirisha bidhaa hiyo kwenda mikoa mbalimbali hapa nchini.
Awali akizungumza Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Tanga Mhandisi Juma Hamsini amesema kuwa pamoja na miradi hiyo bado ipo miradi mingine ambayo itatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani ikiwemo ujenzi wa Barbara, masoko stendi za magari pamoja na mradi wa taa.
"Sisi kama Halmashauri tuna miradi yetu ya ndani ambapo tuna mradi wa soko la Machinga ,tunajenga stendi mpya ya Daladala tutakuwa na sehemu ya kuegesha malori zaidi ya 800 ambayo yote kwa ujumla inaendelea kutekelezwa.
Mhandisi Hamsini amesema kutokana na kutekelezwa kwa mradi wa soko la Makorora tayari Halmashauri imewatengea sehemu ya dharura wafanyabiashara watakaohamishwa eneo hilo ili kuweza kuendelea kufanya shughuli zao ambapo utafanyika mchakato wa kutambua idadi ya wafanyabiashara waliopo.
"Tumezungumza na Mkandarasi ni wapi tutawapeleka wafanyabiashara na wananchi wanaofanya shughuli zao katika soko hili lakini ni lazima tutambue idadi ya wafanyabiashara waliopo na biashara wanazozifanya tutengeneze sehemu ya muda kwaajili kuendelea kufanya biashara zao" alisema Mhandisi Hamsini.
Mradi huo ya ujenzi wa soko la Makorora pamoja na miradi mwingine inatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilion 32 kwa ufadhili wa benki ya Dunia kupitia mradi wa Tactic unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15 ukitekelezwa na Mkandarasi SLEM CONSTRUCTION.
Wakizungumzia ujenzi wa Soko hilo baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Makorora akiwemo katibu wa soko Musa Karata pamoja na Zakati Msumari wamepongeza na kuishukuru Serikali kwani kukamilika kwa ujenzi huo kutawaondolea adha mbalimbali walizokuwa wakikumbana nazo kwa muda mrefu ikiwemo miundombinu mibovu ambayo haikuwa rafiki kwao na hata kwa wateja hali ambayo imekuwa ikiwarudisha nyuma kimaendeleo.
Post A Comment: