SERIKALI imezitaka taasisi zote kuhakikisha angalau watatu kati ya kila watu 20 wanaoajiriwa ni wenye ulemavu, sambamba na kutekeleza masharti ya asilimia mbili za ajira na asilimia tano ya zabuni za umma zilizotengwa kwa kundi hilo.
Wito huo umetolewa leo Agosti 12,2025jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanayofanyika leo.
“Amani ni kila kitu, tujitahidi kuilinda. Natoa wito kwa taasisi zote kuajiri watu wenye ulemavu, kwani mbali na asilimia mbili zinazotolewa na serikali, kuna asilimia tano kati ya 30 zilizotengwa kwenye zabuni za serikali kwa ajili ya kundi hili. Katika watu 20 mnaowaajiri, hakikisheni watatu kati yao ni watu wenye ulemavu,” alisema Katambi.
Akizungumzia ajira kwa vijana, Katambi alisema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, miradi mikubwa ya kimkakati na programu maalumu za uwezeshaji imefanikisha kutoa ajira kwa vijana milioni 8.
Miradi hiyo ni pamoja na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la Julius Nyerere, Uwanja wa Ndege wa Msalato, pamoja na ajira nje ya nchi. Alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Aidha, serikali inaendelea kubuni fursa mpya kupitia sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, biashara na huduma ili kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kujiajiri na kuajiriwa.
Katika sekta ya biashara na ujasiriamali, vijana 164,443 wamepatiwa mikopo ya masharti nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, huku makampuni 299 yanayomilikiwa na vijana yakinufaika na zabuni za umma zenye thamani ya shilingi bilioni 10.8.
Kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), serikali imetenga ekari 340,244.98 kwa kilimo cha vijana, kuanzisha vituo 16 vya zana za kilimo na kusambaza matrekta 500, ambapo vijana 686 wamenufaika moja kwa moja na vifaa hivyo.
“Zaidi ya vijana 1,240 wameajiriwa kutoa huduma za ugani kwa wakulima, hasa katika mikoa inayolima pamba na korosho. Pia serikali imetoa mikopo ya riba nafuu ya asilimia 4.5 yenye thamani ya shilingi milioni 392 kwa vijana na wanawake 39, huku mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 5.24 ikiwa kwenye hatua za uchakataji,” alisema.
Katika sekta ya mifugo, vijana 158 wamepewa mafunzo ya unenepeshaji wa ng’ombe kupitia vituo atamizi, ambapo ng’ombe 3,285 wamenunuliwa kwa shilingi bilioni 1.5 na kuuzwa kwa shilingi bilioni 2, na hivyo kupata faida ya shilingi milioni 500. Kupitia Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), hekta 7,800 zimetengwa kwa vijana 153 waliomaliza mafunzo hayo.
Sekta ya uvuvi nayo imewanufaisha vijana 500 kupitia mafunzo ya ufugaji wa samaki kwenye vizimba, ufugaji wa jongoo bahari, ukulima wa mwani, unenepeshaji wa kaa na ujasiriamali katika mnyororo wa thamani wa mazao ya viumbe maji.
Post A Comment: