Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yametakiwa kuwa mawakala wa mabadiliko chanya katika jamii kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi.

Wito huo umetolewa leo, Agosti 12, 2025, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, wakati akizungumza katika Kongamano la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali linaloendelea kwa siku ya pili katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Dkt. Jingu alisema mashirika hayo yana wajibu wa kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kifikra na kijamii kupitia miradi mbalimbali wanayoitekeleza.

“Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yamesajiliwa kisheria kwa lengo la kutoa huduma na elimu katika nyanja tofauti kwa jamii. Mtambue kwamba ajenda ya maendeleo endelevu ya taifa ni pamoja na kuwa mawakala wa mabadiliko chanya katika jamii,” alisema Dkt. Jingu.

Aidha, alieleza kuwa mashirika hayo yanapaswa kutekeleza miradi ya uzalishaji iliyo endelevu ili kuondoa utegemezi kwa wafadhili, hususan kutokana na mabadiliko ya sera za nchi za Ulaya na Marekani.

Ameongeza kuwa mashirika yanapaswa kujitafakari upya na kuhakikisha yanatafuta mbinu mbadala za kuendeleza huduma na miradi kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao.





Share To:

Post A Comment: