Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla kusimamia kikamilifu maendeleo ya Mkoa wa Arusha, ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa Kandanda unaojengwa kwaajili ya kutumika kwenye michuano ya Afrika ya Afcon mwaka 2027.

Leo Jumanne Agosti 26, 2025 Chamwino Mkoani Dodoma wakati akimuapisha CPA Makalla pamoja na viongozi wengine aliowateua hivi karibuni, Rais Dkt. Samia kadhalika amewaagiza Wakuu wote wa Mikoa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuzingatia maslahi ya Taifa na  kuhakikisha wanakuwa karibu na wananchi ili kuzijua kero zao pamoja na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja.

"Tumeona haja ya kukurudisha serikalini ili uendelee kutumia ujuzi wako na uzoefu wa kuhudumia wananchi katika ngazi ya Mkoa, Wewe sio Mgeni umeshakuwa Mkuu wa Mkoa Mbeya, Katavi, Mwanza, Jijini Dar Es Salaam na sasa Jiji la Arusha, nina hakika utaliweza vizuri sana. Nakutakia kila la kheri." Amesema Rais Samia.

Aidha Rais Samia pia amekumbusha umuhimu wa Mkoa wa Arusha, akiutaja kama kitovu cha Utalii na Diplomasia nchini, akisema kwa uzoefu wa CPA Makalla ana uhakika kuwa atasimamia masuala hayo na mazingira ya Mkoa wa Arusha kwa ujumla kwa kushirikiana na Viongozi na watendaji wengine ndani ya Mkoa wa Arusha.

Rais Samia pia amemtaka kuhamasisha wananchi wa Mkoa wa Arusha kujiandaa kutumia fursa za kiuchumi za ujio wa mashindano ya Afcon kama sehemu ya kukuza uchumi binafsi na wa Taifa kwa Ujumla. Kwa mara ya kwanza Tanzania, Kenya na Uganda watakuwa wenyeji wa michuano hiyo mwaka 2027 ambapo nchi 24 zinatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo ikimaanisha kuwa maelfu ya watu ikiwemo Wafanyakazi wa vyombo vya habari, makampuni ya udhamini, wapenzi wa mpira, na watalii wa kigeni watakimbilia nchi mwenyeji kwaajili ya tukio hilo, na hivyo kukuza utalii wa ndani na kusisimua mzunguko wa fedha na uchumi katika miji husika.






Share To:

Post A Comment: