Na John Mapepele 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kupandisha hadhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuwa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo.

Aidha, ameitaka Wizara yake kukamilisha taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na  kuitangaza katika gazeti za Serikali kukamilika mara moja.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Agosti 22, 2025  akiwa Bagamoyo katika ziara ya kikazi  katika Mkoa wa Pwani mara baada ya kukagua miradi mbalimbali ya sekta za afya, elimu na miundombinu.

Baadhi ya miradi aliyoikagua ni pamoja na ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi ya Nianjema ambapo amesisitiza kutunza miundombinu hiyo ili iendelee kuwahudumia watoto wengi zaidi.

Amesema lengo la mradi huo ni kuwaweka  pamoja watoto wenye mahitaji maalum ili kuhakikisha wanapata  stadi na ujuzi wa maisha.

Amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maboresho makubwa anayoyafanya nchi nzima katika maeneo ya elimu, afya na miundombinu.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Renatus Kisenha amesema shule hiyo inajumla ya wanafunzi 1688 na inahudumia wanafunzi 65 wenye mahitaji maalum.

Ameishukuru Serikali kwa kutekeleza  mradi huo wa bweni wenye uwezo kuwahudumia  watoto 80.

Amesema  mradi huo umegharimu zaidi ya milioni 141 ambapo ulianzwa kutekelezwa Februari, mosi mwaka jana na kukamilika Julai 15, 2024 na umetekelezwa kwa njia ya force akaunti kupitia mfumo wa kielektroniki wa manunuzi wa NEST.

Pia Mhe. Mchengerwa amekagua ukarabati mkubwa uliofanywa na Serikali katika hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na kuwapongeza watumishi kwa kazi nzuri ya kutoa huduma.

Akisoma taarifa ya mradi huo Mkuu wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Dkt. Kandi Lussingu amesema Serikali ilitoa milioni 900 kwa ajili ya kazi hiyo.









Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: