Na Denis Chambi, Tanga.
MGOMBEA wa kiti cha Ubunge katika Jimbo la Tanga kwa tiketi ya Chama cha National League For Democracy 'NLD' Ramadhani Mwikalo ameeleza shauku yake ya kutaka kufufua viwanda vya mkoa pamoja na zao la Mkonge kuliongezea thamani kwa kulitafutia masoko zaidi nje ya nchi ikiwa ni njia pekee ya kumaliza tatizo la ajira kwa wananchi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo hilo na msimamizi msaidizi wa uchaguzi Jimbo la Tanga Mwanaidi Nondo , Mwikalo amesema kuwa kwa sasa uhitaji wa Mkonge katika masoko ya nje ni mkubwa licha ya uzalishaji wake kuwa mdogo hivyo kuahidi kutafuta masoko pamoja na kushawishi wawekezaji kuja kwa wingi kuwekeza mkoani Tanga.
"Lengo letu kama chama ni moja tu kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Tanga katika nyanja nzima ya maendeleo na endapo nitapata ridhaa kwa nafasi ya ubunge kipaumbe cha kwanza zaidi ni kuhakikisha tunakwenda kuimarisha na kuzidisha kilimo cha zao la Mkonge lakini ukiangalia Kasi yake bado ni mdogo kulingana na uhitaji wa soko uliopo kwa sasa" amesema Mwikalo
"Lakini pia kufufua viwanda vilivyokufa na vilivyopo kuviimarisha vile vilivyopo kuongeza kasi ya uzalishaji lakini kuongeza ushirikiano na wawekezaji waliopo ili tuweze kupata viwanda vingi zaidi" ameongeza Mwikalo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Tanga Abdulkarim Nassoro amesema kuwa chama kinajivunia kumsimamisha Mgombea huyo kwa nafasi ya ubunge ambaye ana utaalumu katika sekta ya uzalishaji ikiwemo viwanda , masuala ya uvuvi pamoja na Madini wakiwa na imani kuwa kupitia nafasi yake itakuwa ni suluhisho la ajira kwa wananchi hususani vijana.
"Tanga tuna matatizo mengi ikiwemo matatizo kwa vijana katika ajira na Mwikalo ni mtaalamu wa masuala ya viwanda, anajua masuala mengi ya uvuvi na Tanga tumezungukwa na Bahari changamoto yake itakuwa imefiki utatuzi, tuna matatizo ya Barabara yetu yaTanga Pangani , Ramadhani ataisimamia lengo ni kuwa Barabara ya mfano katika kiwango cha lami tunayo maeneo mengi ya Madini pia Mgombea wetu atahakikisha hayo yote anakwenda kuyasimamia kwa manufaa ya wananchi" amesema Abdulkarim
Amesema kuwa pamoja na kumpata Mgombea ubunge Jimbo hilo pia limejipanga kwa kuhakikisha linasimamisha wagombea wa udiwani katika kata zote 27 za uchaguzi ambao watakwenda kuishawishi Halmashauri kuongez Kasi ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ili iende ikawe suluhisho la mikopo ya Kausha damu ambayo imekuwa ikiwadhalilisha wananchi hususani wanawake.
"Tutasimamisha wagombea katika kata zote 27 za Jimbo letu la Tanga tena watu wenye mvuto ambao wanaweza kujenga hoja ili waweze kumsaidia Mbunge wetu katika baraza la Halmashauri tunajua udhaifu uliopo kwa madiwani waliopita sasa lazima NLD tuonyeshe chachu kuleta mifumo mwingine wa uongozi" ameongeza mwenyekiti huyo.
Post A Comment: