Na. Farida Ramadhan WF, Dodoma


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Elmaamry Mwamba amewaagiza Wataalam wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali kuhuisha mipango mikakati ya mafungu yao (institutional strategic plans) kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Miaka 25 (Vision 2050), Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) na Mwongozo wa Uandaaji wa Mipango Mikakati unaotolewa na Tume ya Mipango ili kuhakikisha vipaumbele vya taifa vinatekelezwa ipasavyo.

Ametoa agizo hilo jijini Dodoma, katika kikao cha mafunzo ya Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) ulioboreshwa, kufanya Tathmini ya Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2024/25 na Maandalizi ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2025/26.

Dkt. Mwamba alisema ili kuendana na Dira ya Maendeleo mwaka 2050 kuna sera, sheria na vitu vingi ambavyo vinatakiwa vihuishwe kuendana na dira hiyo ni vema mipango na mikakati indaliwe kuendana nayo.

”Nchi yetu inakwenda kuanza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo mwaka 2050, hivyo kuna kazi kubwa ambayo inatakiwa ifanyake kwa wale wanaopanga na kutekeleza mipango, Wizara ya Fedha tunasimamia lakini wanatekeleza na kusimamia ni nyinyi, ni wakati muafaka wa kuangalia dira hiyo inasema nini hasa katika maeneo yetu ili tuweze kuandaa nayo “ alibainisha Dkt. Mwamba.

Alisisitiza wataalam hao kuandaa na kuhakikisha wanatekeleza mipango na bajeti kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaasisi, vya kisekta na vya kitaifa ili kuepuka uhamisho wa fedha usio wa lazima.

Aidha, Aliwaagiza kuzingatia Sheria ya Bajeti SURA ya 439 na Kanuni zake wakati wa uandaaji na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali na sheria zingine zinazohusu uandaaji na utekezaji wa bajeti ya Serikali kama vile Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kuhakikisha bajeti inatekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali.

Dkt. Mwamba pia aliwaagiza kuzingatia Maelekezo yanayotolewa kwenye Mwongozo wa uandaaji wa Mpango na Bajeti inayotolewa kila mwaka wakati wa maandalizi ya mpango na bajeti, pamoja na Maelekezo yanayotolewa kwenye waraka wa Hazina namba 1 wa mwaka 2025/26 kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26.

Kwa upande wa washiriki wa kikao hicho walisema mafunzo hayo yamewawezesha kupata ulelewa mambo mbalimbali katika undaaji na utekelezaji wa Bajeti huku wakitilia mkazo wa kutekeleza kikamilifu maagizo yaliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ili kuhakikisha bajeti inatekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Bw. Said Mabie ni miongoni mwa washiriki hao ambaye alisema mafunzo hayo yamewawezesha kuhakikisha hawatengi fedha katika miradi ambayo haina matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi.

Kikao hicho cha siku tano kilianza mwanzoni mwa Wiki hii kwa kutoa mafunzo ya Mfumo wa CBMS ulioboreshwa na kuendelea na tathmini ya utekelezaji pamoja na uandaaji wa bajeti ya Serikali ili kupata maoni yatakayosaidia katika maandalizi ya Mwongozo wa uandaaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2026/27
Share To:

Post A Comment: