Ahadi ya Serikali ya kufikisha umeme wa gridi ya taifa katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera imetekelezwa baada ya Serikali kusaini mikataba ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benako, Ngara  hadi Kyaka  wilayani Misenyi na kituo cha kupoza umeme cha Benako cha msongo wa kilovoti 220/33, hatua inayotoa uhakika kwa Mkoa huo sasa kupata umeme wa gridi badala ya kutegemea umeme kutoka Uganda kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini kwa mikataba hiyo jijini Dodoma tarehe 25 Agosti, 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa kuanza kutekelezwa kwa mradi huo ni moja ya maelekezo ya Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa na kiu ya kutekeleza ahadi ya Serikali kwa wananchi wa Kagera  ya kupata umeme wa uhakika muda wote ili kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii.

" Kupitia mradi huu, Mkoa wa Kagera kwa mara ya kwanza na wenyewe unaingia kwenye gridi ya Taifa hasa na hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme hususan katika Wilaya za Bukoba, Muleba, Misenyi, Karagwe, Kyerwa  na maeneo mengine ya jirani, nawahakikishia watu wa Kagera kuwa Serikali imeshaamua mradi  huu ufanyike kwa wakati kwa  miezi 24 tu" Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amesema, Kagera ambayo mahitaji yake ya umeme hayazidi megawati 47 baada ya muda itakuwa na uhakika mkubwa wa upatikanaji umeme kwani kutakuwa na njia mbalimbali za kufikisha  umeme mkoani humo ikiwemo Benako- Karagwe hadi Kayaka,  Nyakanazi- Biharamulo hadi Muleba na kuna mradi mwingine mkubwa  unaotarajiwa kujengwa kutoka Ibadakuli hadi Mbarara Uganda wa kV 400. Vilevile kuna mradi wa uzalishaji umeme wa Kakono wa megawati 87 ambao upo katika hatua za mwisho za kutafuta Mkandarasi.

Ameongeza kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pia anaendelea kutekeleza miradi mingine ya umeme katika maeneo mengine ikiwemo mradi wa usafirishaji umeme wa kV 400 wa Tanzania- Zambia, mradi wa Usafirishaji umeme wa kV 400 Chalinze-Dodoma , mradi wa usafirishaji umeme wa Mkuranga -Pwani ambao utapeleka  umeme kwa wananchi wa Kusini, pia mradi wa usafirishaji umeme wa gridi imara wa Tunduru- Masasi- Mahumbika ambao pia unaenda kutoa uhakika wa umeme katika mikoa ya Kusini.

" Utekelezaji wa miradi hii yote ya umeme ni kielelezo kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaonesha njia ya kuwafikishia wananchi umeme wa uhakika sasa kinachohitajika kwa watendaji ni kukimbia badala ya kutembea kwani kinachotakiwa ni matokeo na siyo kusema sana." Amesisitiza Dkt. Biteko

Pia Dkt. Biteko amewashukuru wafadhili wa mradi  ambao wametoa Dola za Kimarekani takriban milioni 105.6 ambazo ameagiza kuwa zitumike kwa usahihi ili kuwapa sababu wafadhili wengine kuendelea kusaidia miradi mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameagiza TANESCO kuhakikisha wananchi 1,014 wanaopisha mradi wanalipwa fidia yao  mapema iwezekanavyo yaani kuanzia mwezi septemba mwaka huu.

Aidha, amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na watendaji wa  TANESCO  kwa kuendelea kusimamia kwa umakini Sekta ya Nishati.

Vilevile, ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kuboresha utendaji wake na kwa kusimamia  haki hasa pale zabuni zinapotangazwa. Aidha ametaka mipango iliyowekwa kwenye mradi huo iheshimiwe ili thamani ya fedha ionekane na wananchi wapate huduma kwa wakati.

Dkt. Biteko ameomba wananchi mkoani Kagera kuchangamkia fursa kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika mara baada ya miradi itakayofikisha umeme mkoani humo kukamilika.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa amepongeza Serikali  kwa kuona umuhimu wa kutekekeza mradi huo wenye gharama kubwa ikiwa ni kuonesha kwa vitendo jinsi inavyowajali wananchi hao.

Amesema wilaya zote mkoani Kagera zitaunganishwa na gridi kwani kwa  sasa no wilaya tatu tu ndio zimeunganishwa na Gridi ya Taifa.

Ameahidi kuwa, Wananchi katika mkoa huo watakuwa watumiaji wazuri wa umeme na walipaji bili wazuri iili TANESCO iendelee kupata mapato ya kutekeleza miradi mingine.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema  Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa minne ambayo haijaunganishwa kwenye gridi ya Taifa ikiwemo Rukwa, Lindi na Mtwara.

Amesema tukio la  leo ni la kihistoria kwani kukamilika kusainiwa kwa mikataba hiyo kunafanya mikoa yote iliyo nje ya gridi kuwa kwenye mpango wa kupelekewa  umeme gridi hivyo kwa sasa hakuna mkoa ulio nje ya gridi ambao hauna mradi wa kupelekewa umeme.

Amesema kwa sasa Mkoa wa Kagera unapata umeme wa megawati 40 kutoka nchini Uganda kupitia kituo cha Kyaka na megawati 7 kutoka mwekezaji binafsi wa mradi wa Mirongo/ Kikagati.

Amesema wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani jumla ya mikoa sita kati ya 26 haikuwa imeunganishwa kwenye gridi ya Taifa ila kwa kipindi cha minne Serikali imefanikiwa kuunganisha umeme Kigoma na Katavi huku mingine iiliyosalia ikiwa miaradi inayoendelea kutekekelezwa.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANZANIA), Lazaro Twange  mradi huo una umuhimu mkubwa mkoani Kagera kwani wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba Vijijini na Manispaa ya Bukoba kwa muda mrefu sasa zimekuwa  zikiitumia umeme kutoka nchini Uganda takribani megawati 40 kupitia kituo cha kupoza umeme cha Kyaka ambacho kinapokea umeme kutoka Masaka, Uganda kupitia njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 132 kufuatia mkataba wa makubaliano baina ya Tanzania na Uganda.

Pia, kukamilika kwa mradi huo kutawezesha kuunganishwa kwa kituo cha kuzalisha umeme cha Kakono katika Gridi ya Taifa.

Amesema gharama za mradi ni shilingi bilioni 262.5 na utatekelezwa kwa muda wa miezi 24

Amesema.Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za Serikali  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ambapo Mfuko wa Maendeleo wa Shirika la Wauzaji Mafuta Duniani (OPEC)  utachangia dola za Marekani milioni 60, Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi utachangia dola za Marekani milioni 30, Mfuko wa Maendeleo wa Saudia utachangia dola za Marekani milioni 13 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itachangia dola za Marekani milioni 2.6 kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi.

Amesema Wakandarasi watakaotekeleza mradi huo ni kampuni ya M/s. TBEA Co. Ltd kutoka nchini China ambayo itahusika na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Benako, na Kampuni ya M/s. Transrail Lighting Limited kutoka India itahusika na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Benako hadi Kyaka.









Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: