Na. Peter Haule, WF, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania na washirika wa Maendeleo wanaochangia Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund), wamesaini Hati ya makubaliano ya kuchangia katika Mfuko huo kiasi cha dola za Marekani milioni 55.86 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 161.33 kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Hafla ya kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano hayo imefanyika jijini Dar es Salaam kati ya Makatibu Wakuu wa Wizara ya Fedha, TAMISEMI na Wizara ya Afya na Washirika wa Maendeleo, wakishuhudiwa na Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange.
Akizungumza kwa niaba ya Makatibu Wakuu hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye pia ndiye Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba alisema kuwa makubaliano hayo ya uchangiaji wa fedha kwenye Mfuko wa Pamoja wa Afya ni matokeo ya ushirikiano wa dhati katika kuisaidia sekta ya Afya.
Alisema kuwa misaada hiyo ni mwendelezo wa makubaliano ambayo yalisainiwa mwaka 2021 na yanatarajiwa kumalizika Julai Mosi, 2026 ambapo yataandaliwa makubaliano mengine.
Dkt. Mwamba alisema, kwa niaba ya Wizara ya Fedha na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawashukuru Washirika hao kwa msaada ambao utasaidia katika juhudi za kuboresha sekta ya Afya.
Alisema kuwa vipaumbele vya misaada hiyo, vinaenda sambamba na vipaumbele vya nchi katika Sekta ya Afya na si katika kukuza sekta hiyo pekee lakini pia misaada hiyo inachochea maendeleo kwa wananchi wengi katika nyanja mbalimbali.
Dkt. Mwamba amewataja Washirika wa Maendeleo waliochangia katika Mfuko wa Pamoja wa Afya kuwa ni pamoja na Serikali ya Switzerland, Ireland, Canada, Uingereza, Denmark, Korea, Shirika la Kimataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) na Benki ya Dunia.
Dkt. Mwamba ameahidi kuwa kila msaada utakaotolewa utatumika kwa uwazi na kwa lengo lililokusudiwa ili kuwa na matokeo tarajiwa
Post A Comment: