Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa asilimia 80 ya vifo nchini vinaweza kuzuilika endapo Watanzania wataamua kubadili mtindo wa maisha ikiwemo  kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi ya mara kwa mara.

Amesema hayo tarehe 27 Julai, 2025 jijini Dodoma wakati akimwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika kilele cha msimu wa Sita wa NBC Dodoma Marathon 2025 ambayo imelenga kukusanya fedha kwa ajili ya kuokoa afya ya mama na mtoto.

“Taarifa ya Shirika la Afya Duniani ya mwaka 2022, inaeleza kuwa, mazoezi ya mara kwa mara kama vile kukimbia, yana uwezo wa kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo kwa zaidi ya asilimia 35.Vile vile, mazoezi ya mwili husaidia kujikinga na magonjwa mengine yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, saratani na magonjwa mengine mengi.” Ameeleza Dkt. Biteko

Kwa upande wa Tanzania, Dkt. Biteko amesema kuwa asilimia 33 ya Watanzania watu wazima wana uzito uliopitiliza na asilimia 28 wana shinikizo la damu ambapo ameeleza kuwa magonjwa hayo yanachangia zaidi ya asilimia 40 ya vifo vya mapema lakini asilimia 80 ya vifo hivyo vinaweza kuzuilika kwa kubadili mtindo wa maisha.  

Dkt. Biteko ameipongeza Benki ya NBC kupitia NBC Dodoma Marathon kwa kuunga mkono Serikali katika nyanja mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya kwani katika mwaka 2025 Marathon hiyo imelenga kuendeleza mapambano dhidi ya Saratani ya shingo ya kizazi kwa kushirikiana na  Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Pia, imelenga kutoa ufadhili wa masomo ya Wakunga kupitia Taasisi ya Benjamin Mkapa ili kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi na kutoa ufadhili kwa mafunzo ya Wauguzi  Maalum wa kusaidia watoto wenye changamoto ya usonji (Autism), kwa kushirikiana na AMREF Afrika.

 Vilevile, Dkt. Biteko amesema kuwa tangu NBC Dodoma Marathon kuanzishwa mwaka 2020 imekuwa ni moja ya vilelezo vya  kujenga mshikamano, uzalendo wa kweli na kutatua matatizo mbalimbali katika jamii ikiwemo changamoto za kiafya. 

Dkt. Biteko ameipongeza NBC Dodoma Marathon kwa kuendelea kuimarika kwani mwaka 2024 ilihusisha washiriki 8,000 na mwaka huu imekuwa na  washiriki zaidi ya 12,000 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 50. 

Vile vile, mwaka 2024 NBC Dodoma Marathon ilikusanya kiasi cha Shilingi Milioni 300 huku mwaka 2025 ikikusanya kiasi cha Shilingi Milioni 700 sawa na ongezeko la mapato ya zaidi ya asilimia 133.33.

Amesema kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kama NBC ambao wameendelea kutumia mashindano ya mbio kuimarisha afya za wananchi na kuchangia masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kuokoa afya za watu.

 Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametoa rai kwa Wizara ya Afya, Serikali za Mitaa, Mashirika ya kiraia, Sekta binafsi na wananchi wote  kufanya mbio na mazoezi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ili kuweza kujikinga na matatizo ya afya ambayo wananchi wanaweza kuyapata.

“Nitashukuru sana kusikia kila Taasisi imetenga kwa uchache siku moja kwa mwezi ili kuwa na mazoezi ya pamoja, hii itasaidia kuimarisha afya zetu na kujenga Taifa Imara. “ Amesisitiza Dkt.Biteko     

Vilevile ameipongeza  Wizara ya Afya,  kwa Kampeni ya MTU NI AFYA ambayo inawahamasisha Watanzania kufanya mazoezi kwa angalau dakika 30 kila siku, kula lishe bora, kupima afya mara kwa mara na kujiepusha na tabia hatarishi.

Kwa upande wake, Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema mbio za NBC Dodoma Marathon zimekuwa kivutio kwa wanamichezo wengi kushiriki kutokana na kundaliwa vizuri ambapo amesema kuwa Wizara hiyo itaendelea kuiunga mkono benki ya NBC katika maandalizi ya mbio hizo ambazo zimekuwa na matokeo chanya.

Amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo itaendelea kuweka mazingira mazuri ya wananchi kushiriki michezo mbalimbali pamoja na kuendelea kujenga viwanja vya michezo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Arusha, Dodoma na Dar es Salama ili kuwezesha vijana kujiimarisha kimichezo na kiafya.

 Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi alisema NBC Marathon imekuwa ni moja ya alama za sekta binafsi katika kuwekeza kwenye sekta ya afya  na nyinginezo, akieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano mbio hizo zimefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 1, ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika Sekta ya Afya.

Ametaja mafanikio ya marathon hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu na kufanikisha kupimwa Saratani ya shingo ya kizazi kwa Wanawake zaidi ya 200,000 na kufadhili matibabu kwa wagonjwa 4,800 waliogunduliwa na kansa hiyo katika Hospitali ya Ocean Road.

Amesema, NBC Dodoma Marathon imetoa ufadhili kwa Wakunga 100 katika chuo cha Wakunga Morogoro kwa ushirikiano na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation huku  lengo likiwa ni kufadhili wakunga 500 ifikapo 2028.

Pia ameeleza kuwa, NBC Dodoma Marathon imechangia ujenzi wa Wodi maalum ya Wanawake katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na maeneo mengine katika maendeleo ya sekta ya afya. 

Amesema msimu wa sita wa NBC Dodoma Marathon umehusisha wakimbiaji 12,000 na wamefanikiwa kukusanya shilingi milioni 700 kwa ajili ya afya ya mama na mtoto ikilenga  kuwapatia uchunguzi wa mwanzo wa saratani ya kansa ya kizazi wanawake 10,000, kutoa ufadhili kwa wakunga 100 na kuanzisha mpango mpya wa masomo kwa wauguzi 100 watakaoshughulika na watoto wenye changamoto ya usonji.  

NBC Dodoma Marathon 2025 iliyokuwa na kaulimbiu ya Kata Wese Okoa Maisha imehusisha wanariadha kutoka ndani na nje ya nchi ambapo washindi wamepewa zawadi za jumla ya shilingi milioni 80. Aidha imekabidhi pikipiki 10 kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma.









Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: