NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu, ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa jinsi unavyotekeleza majukumu yake ya kuhakikisha wastaafu wanapatiwa mafao yao kwa wakati.

Ameyasema hayo alipotembelea banda la watoa huduma wa PSSSF kwenye mkutano mkuu wa kwanza wa Maafisa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala (TAPA-HR) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa, AICC jijini Arusha, Julai 24, 2025.

“Katika kipindi cha hivi karibuni ukwasi wa mfuko umeendelea kukua na namna ambavyo mnavyowekeza kimkakati inasaidia Mfuko kuwa himilivu.” Alibainisha.

Pia, amesisitiza PSSSF kuendelea kutoa elimu kwa watumishi wanaokaribia kustaafu ili wanapostaafu mafao wanayopatiwa yaweze kuwa na tija kwao.

Akitoa maelezo kwa Mhe. Sangu, Afisa Mkuu wa Matekelezo PSSSF, Bw. Venance Mwaijibe, alisema tangu kuanza kwa mkutano huo Julai 22, maafisa wa Mfuko wamekuwa wakitoa elimu kwa Maafisa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala kuhakikisha kuwa wanawaandaa watumishi (wanachama ) wawe tayari kustaafu.

“Lakini pia tunawaeleza kuwa huduma zetu kwa sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao kupitia PSSSF Kidijitali, kama vile kusajili wanachama, kuwasilisha madai mbalimbali ya mafao, wastaafu kujihakiki kupitia simu janja lakini pia wanaweza kuuliza maswali yoyote yanayohusiana na uanachama.” Alisema Bw. Mwaijibe.

Mkutano huo ambaoi umewaleta pamoja maafisa haom kutoka bara na visiwani, unafikia kilele Julai 25, 2025 ukiwa umebeba kaulimbiu isemayo ‘Mwelekeo mpya wa nafasi ya wataalamu wa usimamizi wa rasilimali watu na utawala kusukuma mabadiliko kuendana na mageuzi ya teknolojia’.

Share To:

Post A Comment: