Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe ametoa wito kwa Watanzania kuweka jitihada za pamoja katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Dkt. Magembe amebainisha hayo leo tarehe 24, Julai, 2025 Jijini Arusha katika Kikao cha sekta mbalimbali Bara na Visiwani cha usimamizi wa Mradi wa Mfuko wa Pandemic unaosaidia kujiandaa kukabiliana na Magonjwa ya mlipuko(Pandemic Fund) kilichoratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani(WHO).
Dkt.Magembe amesema ni muhimu kwa kila mmoja kuweka jitihada katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa kuzingatia kanuni za afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
"Ujumbe wangu kwa Watanzania ni lazima wachukue tahadhari, magonjwa mengi ya mlipuko yanazuilika endapo utachukua tahadhari,Kipindupindu kinazuilika endapo utazingatia kanuni za afya , matumizi ya vyoo, kuepuka kujisaidia ovyo,kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni lakini magonjwa kama Mpox yanazuilika kwa kuepuka misongamano na kugusana na mtu aliyeonesha dalili za ugonjwa huo.
Akizungumzia kuhusu mfuko wa Pandemic Fund Dkt. Magembe amesema Mfuko huo umekuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
"Serikali kwa kushirikiana na Wadau tuliomba fedha kupitia mradi wa "Pandemic Fund kwa ajili ya kusaidia nchi yetu iweze kujiandaa kukabiliana na majanga yanapotokea na kuimarisha mifumo ya afya,tunashukuru uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha mradi huu kuja Tanzania ambao utatekelezwa Tanzania Bara pamoja na Zanzibar kwani utatuwezesha kuandaa wataalamu wetu, mifumo ya kugundua magonjwa kabla hayajatokea na maabara zetu na uratibu wa pamoja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu"amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Makame Khatib Makame amesema Mradi wa Pandemic Fund utaleta tija kubwa katika uratibu wa pamoja katika utekelezaji wa dhana ya afya moja hasa tahadhari za pamoja.
Mkurugenzi Msaidizi Afya Moja , Idara ya Usimamizi wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt.Salum Manyatta amesema Pandemic ** Fund utakuwa wa miaka mitatu na utakuwa na tija kubwa katika kujiandaa mapema kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika Sekta ya Afya .
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani(WHO) Dkt.Galbert Fedjo amesema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na Magonjwa ya mlipuko ambapo kupitia mradi wa Pandemic Fund utakuwa na mchango mkubwa kujiandaa kukabiliana na magonjwa.
Ikumbukwe kuwa utekelezaji wa bajeti kuhusu Pandemic Fund kazi zimegawanywa kulingana na washirika wa maendeleo kama ilivyoelekezwa katika uandishi wa andiko ambapo kazi zote za afya ya binadamu zinaratibiwa na WHO, afya ya mifugo zinaratibiwa na FAO na za Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii -UNICEF ambapo kulingana na mwongozo wa PF mratibu wa Jumla ni WHO akishirikiana na Wizara ya Afya na kiasi cha mradi ni zaidi ya Tsh.63,746,321,925.
Post A Comment: