Na Munir Shemweta, WANMM

 

Serikali imesema kuwa, mafunzo ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Burundi yanalenga kujenga uelewa wa pamoja kati ya wataalamu wa nchi hizo mbili.

 

Hayo yamebainishwa leo tarehe 22 Julai 2025 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Burundi.

 

Kwa mujibu wa Mhandisi Sanga, mafunzo hayo ya wataalamu wa nchi hizo pia yataharakisha kasi ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Burundi.

 

"Mafunzo haya ni matokeo ya kikao cha uimarishaji mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Burundi kilichofanyika Gitega nchini Burundi kuanzia tarehe 4-7 April 2025 ambapo nchi hizo mbili zilikubaliana kuwa na mafunzo ya pamoja ya kujenga uelewa wa pamoja ili kuharakisha kasi ya uimarishaji mpaka" amesema.

 

"Wakati mwingine kama hamna uelewa wa pamoja mnaweza mkafika uwandani mkaanza kubishana, kunaweza kukawa na mabishano uwandani lakini mkiwa na uelewa wa pamoja uimarishaji unafanyika vizuri" amesema mhandisi Sanga

 

Aidha amesema kuwa baada ya mafunzo hayo kazi ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Burundi itakamilika kwa wakati na kusisitiza kwamba mipaka ipo na unapofanyika uimarishaji mipaka ni pale panapotokea uharibifu.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Hamdouny Mansoor amesema, nchi hizo zilikubaliana katika kikao chao ili kujenga uelewa wa pamoja wakutane eneo moja na kupata mafunzo na baada ya hapo kwenda uwandani kuimarisha mpaka.

 

"Kupitia haya mafunzo tutakuwa na uelewa wa pamoja na pale tunapokuwa tunaandaa ramani ya mwisho itakayoandaa mpaka wetu na kuja kujumuishwa kwenye hifadhi ya mpaka utakaofanyiwa marejeo tutakuwa na alama zinazotambulika na pande zote, huo ndiyo msingi mkuu wa mafunzo haya" amesema

 

Kwa mujibu wa Mansoor, mafunzo yanayofanyika yatagusa maeneo makuu manne aliyoyataja kuwa ni uwekaji vipimo, uwekaji alama katika ramani, masuala ya mikataba pamoja na upigaji picha za anga utakaowezesha kufanya tafsiri za kubaini mpaka kwa kutumia picha za anga.

 

Kiongozi wa ujumbe wa Jamhuri ya Burundi Bw. Niyonkuru Apollinaire amesema, mafunzo hayo yataharakisha uimarishaji mpaka wa Kimataifa kati ya nchi yake na Tanzania kwa lengo la kuzifanya alama za mpaka kuonekana kwa usahihi na kusisitiza kuwa, nchi hizo kwa sasa zinao ushirikiano mzuri.

 

Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya umoja wa Afrika kuwa ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.

 

Tanzania imepakana na nchi 10 ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, DRC, Zambia, Malawi, Msumbiji, Comoro na Shelisheli huku mipaka baina ya nchi hizo ikiwa imegawanyika katika sehemu mbili za nchi kavu na majini.








Share To:

Post A Comment: