Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa matibabu ya ubingwa bobezi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia uwezo wa wataalamu wa ndani ya nchi.

Makubaliano hayo yalisainiwa jana katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma na Wakurugenzi watendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na BMH.

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama alisema ni jambo la kupendeza kuona wataalamu waliopo ndani ya nchi wanasaini makubaliano ya kujengeana uwezo wao kwa wao na kutotegemea wataalamu kutoka nje ya nchi.

Mhe. Mhagama alisema siku za nyuma walikuwa wanawategemea wataalamu kutoka nje ya nchi kuja kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani ya nchi lakini sasa hivi mambo yamebadilika wataalamu wa ndani wanajengeana uwezo wao kwa wao na kuna wataalamu wanatoka nje ya nchi wanakuja kujengewa uwezo hapa nchini.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika majengo, vifaa tiba vya kisasa na kusomesha wataalamu wa afya kitu kilichosababisha huduma za matibabu ya ubingwa bobezi kupatikana hapa nchini”, alisema Mhe. Mhagama.

Aidha Waziri huyo wa Afya alisema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya Afya na Tanzania kupokea wagonjwa kutoka nje ya nchi ambao wanakuja kutibiwa, wakati umefika sasa kwa Hospitali zinazotoa huduma za ubingwa bobezi kuimarisha Utalii Tiba na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa kufuata miongozi ya afya kwa wagonjwa wanaowahudumia.

“Nimepokea ripoti ya kambi maalumu ya matibabu iliyofanyika Visiwani Comoro ambayo ilishirikisha wataalamu kutoka JKCI, BMH, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Taasisi ya Saratani Ocean Road, ninawaomba muendelee kuungana  kwa pamoja kama mlivyofanya Comoro muende katika nchi nyingine kutoa huduma za ubingwa bobezi ili wale mtakaowakuta na shida waje kutibiwa hapa nchini”,alisema Mhe. Jenista.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema ushirikiano uliokuwepo baina yao na BMH umesaidia kuimarika kwa upatikanaji wa huduma ya matibabu ya moyo hapa nchini.

“Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wamekuwa wakiwajengea uwezo wataalamu wa magonjwa wa moyo waliopo BMH kwa kufanya hivi upatikanaji wa huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo umeongezeka na kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa uharaka”, alisema Dkt. Kisenge.

Akikabidhi taarifa ya kambi maalumu ya matibabu ya ubingwa bobezi wa magonjwa mbalimbali iliyofanyika Visiwani Comoro Dkt. Kisenge ambaye alikuwa mratibu wa kambi hiyo alisema waliona zaidi ya wagonjwa 2700 na wagonjwa zaidi ya 400 walishafika hapa nchini kutibiwa na wameingiza zaidi ya shilingi bilioni 3.

“Mwishoni mwa mwaka jana tulienda Visiwani Comoro kuwatibu wenzetu ambao wanatutegemea Tanzania kupata huduma za ubingwa bobezi, tukiwa nchini humo tuliwajengea uwezo wataalamu wao na kujenga ushirikiano baina ya hospitali zao na zetu”, alisema Dkt. Kisenge.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) Prof. Abel Makubi alisema ushirikiano wa BMH na JKCI ulianza miaka mingi iliyopita lakini sasa hivi wameona wauweke katika maandishi.

“Tutaendelea kushirikiana katika kufanya tafiti za magonjwa ya moyo, kutoa mafunzo kwa wataalamu wetu na kubadilishana ujuzi wa kazi hii ikiwa ni pamoja na kufanya matibabu ya pamoja”, alisema Prof. Makubi.

Katika hafla hiyo ya utiaji saini makubaliano hayo ambayo ilikwenda sambamba na uzinduzi wa kliniki ya wagonjwa wa kimataifa, wagonjwa maalumu na uchunguzi wa afya katika Hospitali ya Benjamini Mkapa Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama alimteua Dkt. Peter Kisenge Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kuwa Mwenyekiti wa kamati ya Utalii Tiba nchini.

Share To:

Post A Comment: