Na Dixon Busagaga Moshi
Katika hali isiyo ya kawaida lakini yenye mafunzo kwa jamii,
mkazi wa Kijiji cha Maendeleo wilayani Moshi, Yusufu Samweta, ameeleza namna
zawadi ya jiko la umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ilivyobadili
maisha ya familia yake — si tu kwa kupunguza gharama za upishi, bali pia kwa
kumaliza migogoro ya kifamilia iliyokuwa imeshamiri nyumbani kwake.
“Tulikuwa tunagombana na mke wangu kwa sababu chakula
kilichelewa — moshi mwingi, kuni hazipatikani kwa wakati, watoto wanalia.
Lakini tangu TANESCO waletee hili jiko, maisha yamebadilika. Tunakula kwa
wakati, hakuna kelele, hakuna ugomvi… hata afya imeimarika,” alisema Samweta
kwa hisia.
Kauli hiyo imekuja kufuatia kampeni ya TANESCO ya kusambaza
elimu na vifaa vya matumizi ya nishati safi kwa wananchi, kupitia ushiriki wake
kwa wanawake shupavu ikiwa ni sehemu ya kukutana na wanawake hao Agosti itatu
mwaka huu katikamkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Afisa Uhusiano Huduma kwa
Wateja wa TANESCO Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Mwanaisha Mbita, alisema kuwa
lengo ni kutumia fursa ya tkuwawezesha wananchi kupata elimu ya matumizi ya
nishati salama na kuhamasisha mabadiliko ya kijamii kupitia teknolojia rafiki
kwa mazingira.
“Tunataka kuona wanawake na familia kwa ujumla wakijifunza
kutoka kwa akina kina Samweta — kwamba jiko la umeme linaweza kuokoa muda,
kuboresha afya, kuondoa migogoro ya kifamilia na pia kusaidia kutunza
mazingira. Tunaamini nishati safi ni msingi wa maendeleo endelevu,” alisema Bi.
Mbita.
Bi. Mbita aliongeza kuwa TANESCO inaendelea kutoa majiko ya
mfano kwa baadhi ya familia ambazo bado hazijaanza kutumia umeme kwa ajili ya
mapishi, huku ikiwapa mafunzo ili wawe mabalozi wa mabadiliko katika vijiji
vyao.
Takwimu kutoka TANESCO zinaonesha kuwa nishati ya umeme ni
nafuu zaidi kwenye matumizi ya upishi ikilinganishwa na mkaa au gesi, na pia ni
salama kwa mazingira, hivyo kuchangia juhudi za kitaifa za kupunguza ukataji wa
miti.
Kwa familia ya Samweta, jiko hilo limekuwa zaidi ya kifaa cha kupikia — limekuwa nyenzo ya amani, afya bora na mshikamano wa ndoa.
Post A Comment: