Na. Josephine Majura, WF, Dodoma


Wanawake wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi kushiriki na kupiga kura katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kifanyika mwezi Oktoba mwaka huu ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia.

Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Fedha, Bi. Fauzia Nombo, wakati akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, katika hafla ya kikundi cha wanawake wa Wizara cha Golden Women, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mabele jijini Dodoma.

Bi. Fauzia alisema kuwa ni muhimu kwa wanawake kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya kwa kuendeleza misingi ya heshima, uadilifu, kujituma na kupenda kazi, huku wakitenga muda wa kutosha kwa ajili ya kulea familia zao kwa maadili bora.

“Kundi hili la wanawake ni shupavu, mnavuka mipaka ya kawaida na mnaamua kufanya kazi kwa bidii kujenga uchumi wa taifa kwa mikono na akili zenu. Muendelee kujifunza, kulinda ndoto zenu na kusonga mbele bila kurudi nyuma,” alisema Bi. Fauzia.

Aidha, alilipongeza Kundi hilo kwa kuwaleta pamoja wanawake wa Wizara hiyo kushiriki masuala ya kijamii na kiuchumi bila kujali vyeo au nafasi zao kazini, hali inayoongeza morali ya utendaji kwa watumishi wanawake.

Bi. Fauzia pia alisisitiza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mfano bora wa mwanamke jasiri na kiongozi wa kupigiwa mfano kutokana na juhudi zake za kuhakikisha amani, utulivu na ustawi wa uchumi wa nchi vinaendelea kuimarika.

“Mhe. Rais ameonesha ukakamavu na ujasiri wa hali ya juu katika kuongoza Taifa hili na ni jambo kubwa la kujifunza kutoka kwake,” alisema Bi. Fauzia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Golden Women Group, Bi. Consolatha Maimu, alisema lengo la Kikundi hicho ni kudumisha umoja, mshikamano, kufarijiana, kusaidiana katika shida na raha na kutoa misaada kwa makundi yenye uhitaji.

Nao, baadhi ya wanachama wa kikundi hicho, Bi. Zawadi Ngonde na Josephine Gasule walisema kupitia umoja huo wamepata mafunzo mbalimbali kuhusu nafasi na mchango wa mwanamke katika maendeleo ya familia na Taifa.

Kikundi cha Golden Women, kilianzishwa Julai 2023, kikiwa na jumla ya wanachama 381, wakiwa ni watumishi wanawake wa Wizara ya Fedha na waliowahi kuwa watumishi wa Wizara hiyo ambao wapo kwenye Taasisi nyingine.






Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: