Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Leo Jumapili Juni 15, 2025 Jijini Dodoma, amesema Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania anatekeleza majukumu yake vyema na mafanikio yanaonekana na Kila Mtanzania, akiahidi kuendelea kusimamia na kutekeleza maelekezo yake ili kufikia malengo waliyojiwekea.

"Nikupongeze kwa kutekeleza majukumu yako vizuri, kwa mafanikio na tunaona maendeleo ya nchi yanaendelea kupaa. Jana ulikuwa na kazi kubwa ya kukagua mradi wa kimkakati wa ujenzi wa uwanja wa ndege Msalato lakini pia barabara ya mzunguko Dodoma, barabara ambayo itaondoa msongamano katikati ya Jiji. Haya yote ni miongoni mwa mambo makubwa, mazuri unayoendelea kuyafanya nchi hii.", amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Mhe. Majaliwa pia amezungumzia ujenzi mkubwa wa daraja la Kigongo- Busisi Mkoani Mwanza ambalo linatarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia mwanzoni mwa Juma lijalo, akibainisha kuwa ni miongoni mwa miradi mikubwa iliyosimamiwa na kukamilishwa na serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia.

Wakati wa kuapishwa kwa Jaji Mkuu mpya wa Tanzania Mhe. George Masaju, Waziri Mkuu Majaliwa pia amemshukuru Jaji Mkuu mstaafu Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa ushirikiano na mageuzi makubwa aliyofanikisha kwenye muhimili wa mahakama ya Tanzania, akiahidi pia kushirikiana na Jaji Mkuu mpya Mhe. George Masaju katika usimamizi na uendelezaji haki nchini.

Awali katika maelezo yake, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amewataka watanzania kusoma na kuielewa vyema Katiba ya Tanzania hasa katika nafasi na Majukumu ya Rais wa nchi, akieleza kuwa Katiba inamtambua Rais kama Mkuu wa nchi na Mkuu wa serikali na anapokuwa Mkuu wa nchi, mihimili yote ya dola inakuwa chini yake na ndiyo sababu ya kufanya kazi na mihimili yote ya Dola iliyopo nchini.

Share To:

Post A Comment: