Jaji Mkuu aliyemaliza muda wake Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwezeshaji wake mkubwa katika muhimili wa Mahakama ya Tanzania, akimtaja kama Kiongozi imara mwenye kutambua kuwa utoaji wa haki ni sehemu muhimu ya maendeleo ya nchi.

Jaji Mstaafu Prof. Juma ameeleza hayo leo Jumapili Juni 15, 2025 Jijini Dodoma, wakati wa kuapishwa kwa Jaji Mkuu mpya wa Tanzania Mhe. Geoge Masaju, akieleza kuwa uwezeshaji mkubwa uliofanywa ndani ya Mahakama kwa miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia umekuza ufanisi na utulivu ndani ya Mhimili huo.

"Ukisikiliza mitandao ya kijamii, wana tafsiri hasi ya uhuru wa Mahakama, wengi wanadhani ule ushirikiano na mihimili mingine inaingilia uhuru wa mahakama, sio kweli kwasababu wewe unachotafuta katika ushirikiano ni rasilimali ya Taifa ambayo inasimamiwa na mihimili mingine, hicho ndiyo unakitafuta na hata siku moja, Mimi sijawahi kukaa na Rais, Spika na Waziri Mkuu tukawa tunaongelea mambo ya kesi, siku zote tunaongelea mambo ya maslahi makubwa." Amebainisha Prof. Juma.

Prof. Juma ameeleza kuwa bila ushirikiano huo hakuna ambacho kinaweza kufanywa na Mahakama, kwani kulingana na Taratibu, Rais wa nchi pamoja na Bunge ndiyo wawezeshaji wakubwa wa bajeti, rasilimali fedha, rasilimali watu pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa kupitia sheria ya usimamizi wa mahakama ambayo imekuwa kiungo muhimu katika kuimarisha uhuru wa Mahakama.

Aidha Prof. Juma, Jaji wa 9 wa Mahakama ya Tanzania, mbali ya kumpongeza na kumtakia kheri Jaji Mkuu mpya, Amesisitiza umuhimu wa kukamilisha miradi yote iliyoanza kutekelezwa na Mahakama ikiwemo Ujenzi wa Mahakama za mwanzo 72, Mahakama za Wilaya 12 pamoja na majengo tisa ya Vituo Jumuishi vya utoaji haki nchini ambapo tayari serikali ya awamu ya sita ilishatoa fedha za kukamilisha ujenzi huo.

Share To:

Post A Comment: