WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohammed Mchengerwa amezivunja kamati zote za Halmashauri kuanzia 20 Juni, 2025, hadi pale uchaguzi mpya wa Madiwani utakapofanyika.
Kutokana na hilo,Masuala yote ya kiutendaji katika Halmashauri yatasimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kipindi cha mpito, akisaidiana na Wakuu wa Idara kama wajumbe wa kamati.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 15,2025 Jijini Dodoma wakati akizunguzungumza na Waandishi wa Habari.
Waziri Mchengerwa amesema , Waziri Mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288, kifungu cha 84A na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287, kifungu cha 178A, amepewa mamlaka ya kuvunja Mabaraza ya Madiwani siku saba kabla ya kuvunjwa kwa Bunge kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Amesema tayari ameishasaini Notisi mbili zinazohusu kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Amezitaja Notisi hizo ni Kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka za Wilaya, 2025 na Notisi ya Kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka za Miji, 2025.
Amesema Notisi hizo zinatarajia kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali siku chache zijazo na zinaelekeza kwamba, vikao vya Halmashauri na Kamati zake zinapaswa ziwe zimekoma siku saba kabla ya kuvunjwa kwa Bunge hapo tarehe 27 Juni, 2025.
“Kwa mantiki hiyo, vikao vya Halmashauri na Kamati zake zinapaswa kuwa zimekoma ifikapo tarehe 20 Juni, 2025.
“Kufanya kikao chochote cha Halmashauri au Kamati yake baada ya tarehe hii tajwa itakuwa ni kukiuka notisi hizo,”amesema Waziri Mchengerwa
Kutokana na hali hiyo Waziri Mchengerwa amezivunja kamati zote za Halmashauri kuanzia tarehe 20 Juni, 2025, hadi pale uchaguzi mpya wa Madiwani utakapofanyika.
Pia Masuala yote ya kiutendaji katika Halmashauri yatasimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kipindi cha mpito, akisaidiana na Wakuu wa Idara kama wajumbe wa kamati.
Amesema Mkurugenzi wa Halmashauri hataruhusiwa,Kuanzisha miradi au uwekezaji mpya na Kubadilisha au kurekebisha mradi, uwekezaji au uamuzi wowote uliopitishwa na Halmashauri kabla ya kuvunjwa.
“Matumizi mabaya ya mamlaka au kutotekeleza kwa ufanisi majukumu ya kiutawala kwa mujibu wa Notisi hizi, kutamfanya Mkurugenzi kuwajibika binafsi kwa mujibu wa Sheria,”amesema Mchengerwa.
Amesema Mkurugenzi wa Halmashauri atawasilisha taarifa ya maamuzi na mwenendo wa vikao vya menejimenti vilivyofanyika wakati wa kipindi cha mpito, katika kikao cha kwanza cha Baraza jipya la Madiwani baada ya uchaguzi.
Aidha,Mchengerwa amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatoa wito kwa wananchi, Viongozi wa Serikali, na Watendaji wote wa Halmashauri kushiriki kikamilifu katika kipindi hiki cha mpito kwa kuzingatia Utawala Bora, Maadili ya Utumishi wa Umma, na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
” Aidha, ninatoa pongezi na shukrani kwa Madiwani wote waliomaliza muda wao wa uongozi kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa,”amesema Waziri Mchengerwa.
Post A Comment: