-Washauriwa kuunda umoja wa kusaidiana na kubadilishana uzoefu
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu ametoa wito kwa waendelezaji wa miradi ya Nishati Jadidifu Mkoani Njombe kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuongeza tija kwenye shughuli zao na kuwa mfano bora kwa waendelezaji wa miradi katika mikoa mingine.
Ametoa wito huo Juni 20, 2025 akiwa katika ziara ya kukagua mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji uliopo katika Kijiji cha Masisiwe, Kata ya Ukwama, Wilaya ya Makete Mkoani Njombe unaomilikiwa na Dayosisi ya Kusini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kupitia Kituo cha Udiakonia Tandala.
"Kwa wingi wa rasilimali ya maji iliyopo Mkoani hapa ni dhahiri uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 50 ndani ya Mkoa huu pekee upo, ni suala la nyinyi waendelezaji wa miradi kuunganisha nguvu kwa kufanya kazi kwa kushirikiana na kusaidiana," alisisitiza Balozi Kingu.
Hata hivyo alipongeza kwa jitihada zinazochukuliwa na waendelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme katika miradi aliyoitembelea na aliwasisitiza kutoridhika na kiasi kidogo wanachozalisha badala yake wafikirie namna ya kutanua wigo wa uzalishaji ili watanzania waweze kunufaika na umeme wanaozalishwa.
Alisema shughuli nyingi zinahitaji umeme na kwamba Taifa linahitaji kuwa na umeme mwingi wenye kutosheleza ili kuwezesha maendeleo ya kichumi na kijamii hasa ikizingatiwa kuwa umeme ni kichocheo muhimu cha maendeleo na ni nguzo ya uchumi.
Aliwakumbusha kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) upo kwa ajili ya kuwaendeleza hivyo wahakikishe wanafanya kazi kwa karibu na Wakala ili kurahisisha shughuli zao na kufikia malengo waliyojiwekea.
"Serikali kupitia REA ipo kwa ajili yenu, hakikisheni kila hatua mnayopiga mnashirikiana kwa karibu na REA ili miradi iweze kwenda kwa kasi na kuleta tija inayokusidiwa," alisisitiza Balozi.
Kwa upande wake Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kusini Kati, Wilson Sanga aliishukuru Serikali kupitia REA kwa kuchangia uendelezaji wa mradi huo unaozalisha kilowati 360 ambazo zote zinaingizwa katika Gridi ya Taifa kwa makubaliano maalum ya kimkataba na TANESCO.
“Tunaishuru sana Serikali kupitia REA kwa kutuwezesha kutekeleza mradi huu ambao umekuwa na mchango mkubwa kwa jamii inayotuzunguka lakini na Taifa kwa ujumla,” alisema Askofu Sanga.
Naye Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage alisema mradi huo wa Ijangala umenufaika na ruzuku ya Jumla ya Shilingi Milioni 996.
Mbali na uwezeshwaji huo, Mhandisi Mwijage alisema Mwendelezaji mradi amewezeshwa na REA kupata mkopo nafuu wa muda wa miaka 12 uliyotolewa kupitia Benki ya Uwekezaji ya Tanzania (TIB) wenye thamani ya Shilingi Milioni 922 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji umeme na utekelezaji wa mradi kwa ujumla.
Mha. Mwijage alisisitiza kuwa milango ya Wakala ipo wazi kwa waendelezaji miradi ya Nishati Jadidifu na kwamba wasisite kuwasiliana na Wakala kwa jambo lolote linalokwamisha uendelezaji wa miradi. Vilevile aliwasisitiza wazalishaji umeme kuhakikisha mazingira yanatunzwa ili kuwa na miradi endelevu.
Post A Comment: