Na Benny Mwaipaja, Dodoma

Tanzania imeondolewa kwenye Orodha ya nchi zenye mapungufu ya kimkakati katika mifumo ya udhibiti utakatishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi, na ufadhili wa silaha za maangamizi (Grey List).

Uamuzi huo umetangazwa na Rais wa Kikosi Kazi cha Kifedha cha Kimataifa (FATF) Bi Elisa de Anda Madrazois, mwishoni mwa Mkutano Mkuu wa FATF uliofanyika katika Mji wa Strasbourg nchini Ufaransa kuanzia tarehe 10 hadi 13 Juni 2025. 

Ikumbukwe kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliorodheshwa kwenye orodha ya nchi zenye mapungufu ya kimkakati katika mifumo ya udhibiti utakatishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi (Grey list) mnamo mwezi Oktoba, 2022.

Wakizungumza kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Mkutano wa FATF, Ujumbe wa Tanzania, ukiongozwa na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu ya Kuzuia Utakatishaji Fedha Haramu, Bi. Sauda Msemo na Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) Bw. Majaba Magana, umeihakikishia FATF na mtandao wa kimataifa kuwa Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha mifumo yake ya udhibiti inabaki kuwa imara.

“Serikali iatendeleza ushirikiano wa kimataifa; na kusimamia maadili ya uwazi, uwajibikaji na utawala bora kwenye mfumo wa kifedha, ambavyo vitachangia kuimarisha usalama wa nchi, kanda, na mtandao mzima wa kifedha kimataifa” alisema Bi. Msemo.

Akizungumzia kuhusu tukio hilo akiwa Dodoma, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) aliishukuru Kamati Ndogo ya Kundi la Afrika kwa ushirikiano katika mchakato mzima, Sekretarieti ya FATF na Kikundi cha Kupambana na Utakatishaji Fedha Haramu Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAAMLG) kwa jitihada kubwa zilizoiwezesha nchi kuondolewa katika grey list na kwamba anatambua na kuthamini msaada wa kitaalam na kifedha kutoka kwa washirika wa maendeleo katika jitihada hizo.

“Tunapenda kuuhakikishia Umma na Jumuiya ya Kimataifa kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amedhamiria kuhakikisha kuwa nchi yetu inabakia kuwa salama dhidi ya vitendo vya uhalifu katika mfumo wa kifedha.” Alisema Mhe. Dkt. Nchemba.

Alisema kwamba nchi itadumisha matokeo mazuri ambayo Tanzania imeyapata na kuendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika mapambano dhidi ya utakatishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi; ili kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa kinara wa uadilifu na uwazi katika mifumo ya kifedha, yenye kujipambanua kwa maendeleo endelevu na ustawi. 

Mhe. Dkt. Nchemba ameitangazia jumuiya za kimataifa kuwa Tanzania ni Mamlaka inayoheshimika na yenye mazingira salama kwa uwekezaji, na fursa kubwa kwa washirikia wa ndani na nje ya nchi katika masuala ya kifedha na kiuchumi kwa ujumla na kuwahimiza wachangamkie fursa hiyo.
Share To:

Post A Comment: