Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake ipo kwaajili ya kustawisha maisha ya wananchi wake, akiahidi kuendelea kuharakisha maendeleo kwenye sekta mbalimbali nchini hasa zenye kugusa maisha ya wananchi walio wengi.

Kauli ya Rais Samia ameitoa leo Jumanne Jioni Juni 17, 2025, wakati wa Mkutano wake wa hadhara Wilayani Itilima Mkoani Simiyu mara baada ya kuzindua Hospitali ya Wilaya ya Itilima, akiwataka kuachana na siasa za zao la Pamba, kwani serikali haitochukua hatua yoyote ya kumdhuru Mkulima.

"Katika kilimo na uzalishaji wa pamba kuna siasa kubwaz niwaombe sana tusikilizeni serikali tunavyowaambia. Serikali hata siku moja haitachukua hatua ya kumdhuru mkulima au mwananchi wake, tutachukua hatua za kunyanyua kilimo na kumfanya Mkulima anufaike na Kilimo chake." Amesema Rais Samia.

Rais Samia katika hotuba yake pia amesema serikali itaendelea na jitihada za kuvutia viwanda Wilayani Itilima na Simiyu kwa Ujumla, akionesha kutoridhika na takwimu za uwepo wa Kiwanda Kimoja kikubwa Itilima, vidogo 9 na vidogo kabusa 92 vilivyoajiri Watanzania 414 peke yake.

"Mwenye uwezo wa kuweka  viwanda vya kuchakata pamba, kukamua mafuta au viwanda vingine nawahamasisha mfanye kazi hiyo. Nawapongeza Halmashauri kwa kutenga maeneo ya viwanda na biashara, hiyo ni fursa nzuri maeneo yatumike na yatarahisisha adhma yetu ya utekelezaji wa kuwavutia wawekezaji ndani ya Wilaya hii." Amekaririwa akisema Rais Samia.

Rais Samia pia amebainisha kuwa serikali ya awamu ya sita inajenga kiwanda kikubwa cha Vifaatiba wilayani humo kitakachohudumia Tanzania nzima, zikitengwa pia Ekari 1,000 kwaajili ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata zao la Pamba Wilayani hapo.

Rais Samia pia amemuelekeza Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega kwenda Wilayani Itilima Mkoani Simiyu kufuatilia ombi la Mbunge wa Jimbo hilo, aliyemuomba Mhe. Rais ujenzi wa barabara ndani ya Wilaya hiyo, akimtaka Waziri Ulega pia kufunga taa kwenye barabara zilizopo wilayani humo.

Share To:

Post A Comment: