Na,Egidia Vedasto, Msumba News
Serikali imeendelea kuboresha sekta ya elimu nchini kupitia mradi wa kuboresha miundombinu ya elimu kwa shule zote nchini (SEQUIP) lengo likiwa ni kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa vya TEHAMA awamu ya pili katika shule ya sekondari Arusha, Naibu Waziri TAMISEMI Zainabu Katimba amepongeza jitihada za maendeleo ya uongozi wa awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mageuzi ya sekta ya elimu.
Aidha amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imeendelea kutekeleza mradi huo wa miaka mitano utakaogharimu jumla ya shilingi Tilioni 1.2 katika manunuzi ya vifaa vya TEHAMA katika shule zote nchini, ujenzi wa maabara, maboresho ya shule zote kongwe, ujenzi wa madarasa mapya, vyoo, mafunzo kwa walimu na kunufaisha shule 231 awamu ya kwanza na shule 422 kwa awamu ya pili kwa nchi nzima.
"Ni dhahiri kuwa, hatua hii ya matumizi ya teknolojia itasaidia kuinua kiwango cha elimu nchini, kuongeza wabunifu na wataalamu katika masuala ya TEHAMA, kuimarisha ushiriki wa kujifunza wanafunzi katika muda wa ziada na kufanyika kwa vipindi mtandaoni".
Katika namna hiyo hiyo, Katimba ametoa maelekezo kwa watendaji wa TAMISEMI wakiwemo Katibu tawala wa mikoa na Wakurugenzi wa halmashauri kusimamia kikamilifu zoezi la ugawaji wa vifaa hivyo ndani ya siku tano tangu kufanyika kwa makabidhiano.
Pia ameagiza shule kuimarisha ulinzi na usalama kwa kuweka milango na madirisha ya chuma, kufanya matengenezo ya haraka pindi vifaa vinapoharibika, kuwepo kwa wataalamu watakaoratibu utunzaji na matengenezo, usafi wa kila wakati kwa vifaa vya TEHAMA na walimu na wanafunzi kutumia vifaa hivyo kwa utaratibu.
Kwa upande wake Mratibu msaidizi wa mradi wa kuboresha elimu ya sekondari nchini (SEQUIP) Mwl. Robert Msigwa amesema utekelezaji wa mradi huo umefanyika kwa miaka minne hadi sasa na kuleta mageuzi chanya katika sekta ya elimu.
Vilevile amebainisha namna Wizara ya TAMISEMI ilivyosimamia vema utekelezaji wa mradi na kufanikisha malengo ya kuongeza udahiri kwa wananfunzi wa kike kwa shule za sekondari kuanzia kidato cha 5-6, kuwapunzia kutembea umbali mrefu, kupunguza idadi ya wasichana wanaobeba mimba shuleni, utoro, na kuwarejesha wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalibmbali.
"Shule takriban 6000 zimenufaika na mradi wa SEQUIP, shule 5000 tayari zimefanyiwa ukarabati, shule 3125 zimepata mafunzo ya elimu salama, ujenzi wa madarasa mapya 830, na walimu wapatao 20,000 kupatiwa mafunzo ya elimu ya TEHAMA" amesema Mwl. Msigwa.
Mkurugenzi wa usimamizi wa elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Emmanuel Shindika amesema mradi huo wa awamu ya pili utanufaisha shule 16 kwa Mkoa wa Arusha.
"Nahimiza vifaa vitunzwe kama inavyotakiwa ili kuwanufaisha wanafunzi wengi zaidi, na kila mmoja atambue kuwa TEHAMA ni msingi wa taifa lolote linaloendelea duniani" ameeleza Dkt. Shindika.
Mmoja wa wanafunzi katika shule ya sekondari Arusha Grace Tarimo ameshukuru ujio wa vifaa vya TEHAMA na kusema utawaongezea kiwango cha ufaulu.
"Namshukuru Rais wetu kwa jitihada zake za kipekee kuhakikisha sekta ya elimu inakua, na tunaahidi tutasoma kwa bidii na kutunza vifaa hivi ili tunufaike kizazi hadi kizazi na kuleta matokeo chanya katika elimu" amesema Grace.
Post A Comment: