Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka ametembelea banda la Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) lililokuwa katika Uwanja wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma, ambako Maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yalifanyika.

Lengo la kutembelea banda hilo ilikuwa ni kujionea na kupata elimu juu ya teknolojia mbalimbali bora za mifugo zinazotokana na tafiti zilizofanywa na TALIRI, ambazo zimekusudiwa kusaidia wakulima na wafugaji kuongeza tija kwa njia endelevu na rafiki kwa mazingira.

Rc Mtaka alipata maelezo kutoka kwa wataalamu wa TALIRI kuhusu mbegu bora za malisho, uzalishaji wa mifugo yenye tija, na mbinu za ufugaji zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi. Vilevile, alielezwa namna taasisi hiyo inavyosaidia kuendeleza sekta ya mifugo kwa kutumia tafiti zenye msingi wa kisayansi.

"Ni muhimu kwa mikoa kama Njombe kunufaika na teknolojia hizi, hasa ikizingatiwa kuwa mifugo ni mojawapo ya sekta zinazochangia pato la wananchi wetu. Ushirikiano wa karibu kati ya watafiti na halmashauri zetu utasaidia kuleta mapinduzi katika sekta ya mifugo," alisema Mhe. Mtaka.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Kuishi kwa Amani na Mazingira Yetu”, yakiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji.

TALIRI ni taasisi ya serikali inayojihusisha na tafiti za kuboresha mifumo ya ufugaji nchini, kwa lengo la kuongeza tija, kipato kwa wafugaji na kuhakikisha uhifadhi wa mazingira.





Share To:

Post A Comment: