Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu Juni 16, 2025 amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuwekeza ndani ya nchi yao ili kukuza uchumi na kuiwezesha nchi kuondokana na utegemezi wa mikopo na misaada kutoka nje ya Tanzania.

Rais Samia amebainisha hayo muda mfupi baada ya kuzindua kiwanda cha kuchakata Pamba na kiwanda cha Mabomba (Moli Oils Mills company), vinavyomilikiwa na kampuni ya NGS vilivyopo Bariadi Mjinj Mkoani Simiyu na vikimilikiwa na Mtanzania kwa zaidi ya asilimia 90 na vikitarajiwa kutoa ajira zaidi ya mia nane kwa watanzania.

Akizungumzia tija ya uwepo wa viwanda hivyo, mbali ya kutoa ajira, Rais Samia amebainisha kuwa Viwanda hivyo vitapunguza matumizi ya fedha za kigeni zilizokuwa zinatumika kuagiza bidhaa nje ya nchi sambamba na kuwezesha utekelezaji wa sera ya serikali ya kuongeza thamani bidhaa mbalimbali ndani ya nchi kabla ya kuziuza nje.

"Nimshukuru mwekezaji hapa wa ndani amewaza kuongeza thamani zao la Pamba kwa hatua ya kwanza lakini kwa hatua ya pili, tutanunua kwake kuweka kwenye kiwanda ambacho tayari tunaanza kukijenga cha kutengeneza nyuzi za pamba, tunataka kusitisha kupeleka pamba yetu kama ilivyo kwenye marobota kwa wenzetu wakatengeneze nguo na watu wao wapate kazi. Tunataka pamba yetu tuitengeneze hapa hapa ili watu wetu wa Simiyu waweze kupata ajira."Amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine Rais Samia amesisitiza dhamira ya kuinua mazao mbalimbali ya biashara nchini ikiwemo zao la Pamba, akiwaomba wananchi wa  mkoa wa Simiyu kukubaliana na hatua zinazochukuliwa kwenye sekta ya Kilimo kwani hakuna dhamira yeyote ya kuweza kuwakandamiza na kuwaumiza wakulima wa Tanzania.

Share To:

Post A Comment: