Mbunge wa Arusha Mjini Mhe. Mrisho Gambo amekuwa miongoni mwa wabunge vijana wa Bunge la Tanzania waliohitimisha kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano cha uwakilishi wa wananchi, akijivunia mafanikio kibao na alama zilizowekwa katika maeneo mbalimbali Jijini Arusha.
Amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa ushirikiano wake mkubwa katika kusukuma maendeleo ya Jiji la Arusha, akieleza kuwa pamoja na mengine, Serikali inajenga uwanja wa mpira wa kisasa kwenye Kata ya Olmot pamoja na viwanja vingine vidogo vitano, kufanikishwa kwa mradi wa TACTIC ambao unajenga barabara ya Engosheraton, Olasiti, Soko la Morombo, Soko la Kilombero na Kituo cha kisasa cha Mabasi eneo la Bondeni City- Wakandarasi wakiwa tayari wamepatikana.
Aidha Gambo amebainisha kuwa ndani ya miaka mitano yake shule mpya 6 za sekondari zimejengwa, Ujenzi wa barabara za lami maeneo ya Mianzini- Ngaramtoni, Ilboru- Kaloleni, Boma Siara- Baraa, Kona ya Kiserian- Moshono, Kijenge Ngulelo- Kimandolu, Kwa Shangazii- Muriet, Kaloleni, Levolosi, TRA- Mochwari-Sekei.
"Tumejenga pia hoja kwa miradi mikubwa ya barabara ya Arusha- Kibaya- Kongwa (KM70) ambayo itajengwa kwa njia nne kutoka Kona ya Mbauda hadi Round about ya Morombo na kumalizia kipande cha Kona ya Kiserian hadi Fun retreat na kukamilisha usanifu wa barabara ya njia nne kutoka Airport hadi Soko la Kilombero." Amesema Mhe. Gambo.
Kadhalika ndani ya miaka mitano, Gambo ameeleza kuwa wamefanikiwa kujenga vituo vya afua Sokoni 1, Olmot na Olasit, kuboresha vituo vya afya Mkonoo, Terrat, Elerai, Levolosi na Kaloleni, pamoja na maboresho ya Hospitali ya Wilaya na Hospitali ya Mkoa pamoja na kuweka nashine za CT Scan na X-Ray mpya 2.
"Tumejenga vivuko na madaraja maeneo mbalimbali Jimboni, tumeboresha uwanja wa ndege Arusha kwa kuongeza eneo la kutua na kupaa, Kujenga maeneo ya kupumzika abiria na kuweka taa ili ndege zifanye kazi saa 24, tumeendelea kusambaza umeme na huduma ya maji maeneo ya pembezoni, kununua mitambo ya kuchonga barabara na malori ya vifusi, Maboresho makubwa kwenye sekta ya utalii pamoja na kurejesha Mikutano toka mwaka 2021 serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani pamoja na utetezi wangu kwa makundi ya kijamii kama Machinga nk." Ameeleza Gambo.
Gambo tayari katika mikutano yake kadhaa na wananchi wa Arusha Mjini alishaonesha nia ya kutetea nafasi yake hiyo kwa kipindi cha pili katika uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.
Post A Comment: