Na, Egidia Vedasto
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amewaaga madiwani waliomaliza muda wao wa halmashauri ya Jiji hilo na kuwataka kuwa mabalozi wazuri wa amani katika maeneo yao.
Akizungumza katika tukio la kuvunja Baraza la Madiwani Jijini humo amesema Madiwani wana uwezo mkubwa wa kulinda na kuhimiza amani kwa kuwa wanawajua vizuri wananchi wao.
Smbamba na hayo, amewataka kuonyesha alama ya matunda ya kazi nzuri zilizofanywa katika kipindi cha awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuchochea maendeleo yaliyomgusa kila Mtanzania.
Hata hivyo ameisitiza stahiki za Madiwani baada ya kuvunjwa kwa Baraza kuwekwa kwa wakati, moja kwa moja kwenye akaunti zao, hii yote ni kutambua mchango wao mkubwa walioutoa katika kipindi chote cha utendaji.
Pia ametumia nafasi hiyo kuwaalika wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani kuja kupata matibabu ya magonjwa yote bure kuanzia tarehe 23-29, yatakayotolewa katika uwanja wa Shekhe Amri Abeid.
"Ushirikiano wenu katika utendaji umechangia kwa kiasi kikubwa katika kuchochea maendeleo ya taifa, kutokana na mema mengi mliyofanya, nawasihi mkawe chanzo cha amani aidha mpate nafasi ya kurudi katika uongozi au hata mkikosa" amesema Makonda.
Akizungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI)Mohamed Mchengerwa amewapongeza Madiwani wote nchini kwa ustadi na umahili katika utendaji kazi wao uliosukuma mbele uchumi wa taifa.
Licha ya hayo amesema kuwa vifaa vyote walivyowezeshwa na serikali katika kipindi chao cha uongozi ikiwemo vishikwambi, wamepewa fulsa ya kuendelea kuvimiliki kwa kuwa vimebeba taarifa zao.
Katika namna hiyohiyo Mkuu wa Wilaya Arusha Joseph Mkude, amewataka Madiwani waliomaliza muda wao kuendelea kudumisha nidhamu na kuisemea serikali kwa wananchi kwa miradi iliyofanywa na serikali kuu.
Aidha amewaahidi kukamilisha miradi yote iliyochelewa kukamilika hadi wakamaliza muda wao wa uongozi, lengo ni kuhakikisha wanaboresha miundombinu na kuchochea maendeleo ya kila mtu.
"Nawatakia kila la kheri katika maisha yenu mapya, lakini pia nawaombea mkafanikiwe katika kampeni ili muweze kurudi tusaidiane kusukuma gurudumu la maendeleo mbele"amesema Mkude.
Vile vile Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe akiahirisha Baraza la Madiwani ameshukuru ushirikiano mkubwa walioonyeshwa kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Madiwani wote katika kipindi chote walichotumikia wananchi.
"Tukumbuke kueleza miradi yote iliyotekelezwa katika kata zetu na serikali ya awamu hii, inawezekana hii ikatusaidia kuongeza kura za wananchi ili tuweze kurudi katika nafasi zetu za udiwani" amesema Iranqhe.
Post A Comment: