MADAKTARI mkoani Tanga, wametakiwa kuenzi na kuzitumia tunu za uadilifu katika utoaji huduma kwa wananchi, ili kufikia lengo la kuwaponya na kuleta nafuu kwa wahitaji. Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ali Ussi, ametoa rai hiyo alipozungumza katika hafla ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa jengo la mionzi la Kituo cha Afya Makorora jijini Tanga. 

Mwenge wa Uhuru wenye ujumbe unaosema JITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU WA 2025 KWA AMANI NA UTULIVU, unakimbizwa kwenye Halmashauri ya Jiji la Tanga utakapotembelea, kukagua, kuweka jiwe la msingi ama kufungua jumla ya miradi saba ya kisekta. Ussi amesema, uboreshaji wa sekta ya afya, kama ilivyo kwenye sekta nyingine kunakosafanywa na Serikali ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan, kunachochea pia uwepo wa mazingira bora kwa watumishi wa umma.

”Kunapokuwa na mazingira magumu kwenye hospitali zetu, hata madaktari hawafanyi kazi zao ipasavyo, hivyo tunapopata jengo la huduma za mionzi kama hili, ni wazi kwamba madaktari wetu wanakwenda kuboresha zaidi utendaji kazi wao,” anasema. Mradi huo uliohusisha vyumba viwili vya kupiga mionzi (X-ray) na ultrasound, unagharimu Shilingi milioni 84.7 za mapato ya ndani, unatekelezwa kupitia fedha za mapato ya ndani ya Kituo hicho. Mradi huo wenye gharama ya Shilingi milioni 84.7 ulianza Oktoba 21, mwaka jana na kukamilika Aprili 24 mwaka huu, ukiwa umetumia njia ya “Force account” na mfumo wa manunuzi kwa njia ya NeST.
Share To:

Post A Comment: