Na, Egidia Vedasto Msumba Blog
Mawakili wa serikali nchini, wamehimizwa kuwa wazalendo na kuzingatia haki katika majukumu yao ya kuitumikia serikali na wananchi wake hususan katika kipindi hiki taifa linapoelekea katika uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa Mawakili hao nchini Jjijini Arusha, Waziri wa Katiba na Sheria Dr. Damas Ndumbaro amewataka Mawakili hao kuzingatia haki, maadili yanayowataka kuepuka rushwa, na kuwakumbusha kujifunza kila siku hatua itakayoongeza weledi na ujuzi katika utendaji wao.
Aidha amewaonya kutojiingiza katika siasa, kwa maaana sheria inakinzana na siasa katika suala la haki. Hivyo ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wanasiasa nchini kutii sheria na kanuni zilizopo katika hatakati zao za kampeni katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
"Kipindi hiki ni muhimu sana katika nchi yetu, katika namna hiyo kasi ya upotoshaji itaongezeka kutokana na ukuaji wa teknolojia uliopo, matumizi ya akili mnemba ambayo wengine wanatumia kufanya uhalifu kwa kubadilisha sauti za watu hususan viongozi wa siasa, nawakumbusha mkawe hodari katika kuikabili teknolojia"amesema Dr. Ndumbaro.
Hata hivyo amewataka kutumia vyema mafunzo waliyopata ili wakaitumikie serikali vyema, kuimarisha ushirikiano na kusaidia Wizara zote kuzungumza lugha moja katika masuala ya sheria.
Kwa upande wake Wakili mkuu wa serikali Dr. Ally Possi amesema mafunzo hayo yatawasaidia Mawakili wa Serikali kuwajengea uwezo wa kutenda kazi kwa maarifa, weledi uadilifu na kwa kwa wakati, na kuzingatia majukumu yao katika nguzo mbalinbali za Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, iikiwemo inayolenga kuwa na Uchumi imara, jumuishi na shindani.
Amesema kupitia nguzo ya "Uchumi Imara, Jumuishi na Shindani" nchi itafikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2050, kuwaongezea elimu katika maeneo mablimbali yatakayosaidia kuweka mazingira wezeshi ya Biashara na Uwekezaji na mabadiliko mtambuka ya kisheria ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
"Shughuli zetu ni kuitetea serikali, katika kutekeleza jukumu hilo katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, Ofisi imeendesha jumla ya mashauri ya madai 9,013, kati ya mashauri hayo, mashauri 8347ni madai ya kitaifa, mashauri 33 ni madai ya kimataifa, na mashauri 633 ni mashauri ya kikatiba na haki za binadamu",
"Katika kuendesha mashauri hayo, mashauri 966 yalimalizika, kati ya mashauri yaliyomalizika mashauri 814 ni ya madai ya kitaifa, shauri moja (01)ni la madai ya kimataifa. Na mashauri 151 ni ya kikatiba na haki za binadamu, Ofisi imefanikiwa kushinda mashauri 750 sawa na asilimia 77.6℅ ya mashauri yaliyomalizika kwa kipindi husika na kuokoa kiasi cha shilingi billioni 51.02 (TZS 51,022, 810, 719.81) kiasi ambacho serikali ingelipa endapo ingeshindwa mashauri hayo" amefafanua Dr. Possi.
Katika namna hiyohiyo Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini, Ofisi ya Wakili mkuu wa serikali Prisca Ulomi amesema Chapa iliyozinduliwa katika mafunzo hayo itasaidia kurahisisha utendaji wa shughuli za ofisi, kusimamia maadili ya Mawakili, katika namnaya uvaaji na muonekano wao, namna ya kufanya mawasilisho mbele ya mahakama na taswira wanavyotakiwa kuwa nayo itakayowatambulisha kitaifa na kimataifa.
Mafunzo hayo yamejumuisha Mawakili zaidi ya 600 kutoka Wizara zote nchini, Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali bara na Visiwani, Taasisi za umma, Wakala za serikali, Mashirika ya umma, Mamlaka za udhibiti na vyuo nbalimbali nchini na kubeba kaulimbiu "Ubobezi wa Kisheria kwa ajili ya Kesho: Teknolojia, Mikakati na Mizania ya Maisha kwa Mawakili wa Serikali katika Kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050".
Post A Comment: