.
Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imepongeza utendaji bora wa Shamba la Miti la West Kilimanjaro, huku ikielezea kuridhishwa na namna linavyoboresha maisha ya wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia uzalishaji endelevu wa mazao ya misitu.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Meja Jenerali Dkt. Mbaraka Mkeremy, wakati wa ziara ya kikazi iliyofanyika Juni 24, 2025, Mjumbe wa Bodi Dkt. Siima Bakengesa alisema kuwa Shamba hilo limeonyesha mfano wa kuigwa katika kuendeleza rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi na kizazi kijacho.
"Tumefurahishwa na kazi nzuri inayofanyika hapa West Kilimanjaro. Tumeona namna shamba hili linavyochangia pato la Taifa kupitia uzalishaji wa miti na pia kuwanufaisha wananchi kwa kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama kilimo na ufugaji wa nyuki,” alisema Dkt. Bakengesa.
Dkt. Bakengesa alisifu uwekezaji unaoendelea kufanyika katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi, ukarabati wa majengo na uboreshaji wa miundombinu ya msingi.
"Tunapongeza juhudi za TFS katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi. Haya ni mambo muhimu yanayochochea ufanisi na kuongeza motisha kazini,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo, Bw. Robert Faida, alieleza kuwa shamba hilo limeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya uwekezaji kwa kushirikiana kwa karibu na makao makuu ya TFS.
"Katika miaka ya hivi karibuni, tumeimarisha huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na miundombinu ya makazi, vitendea kazi, na ushirikiano na jamii. Tunaendelea kuboresha zaidi kwa kadri rasilimali zinavyoruhusu,” alisema.
Akizungumzia nafasi ya sekta binafsi katika kuendeleza misitu, Bw. Faida alihimiza wawekezaji kuanzisha viwanda vya kisasa vya kuchakata mazao ya misitu, huku akieleza kuwa mahitaji ya mbao nchini yanaendelea kuongezeka na kutoa fursa pana kwa uwekezaji.
Post A Comment: