Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameunda timu ya wataalamu na kuipa siku saba kuchunguza changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika Kivuko cha MV TANGA kilichopo wilayani Pangani, mkoani Tanga baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu kusuasua kwa utendaji wake.

Pia, katika ziara yake mkoani Tanga, Ulega pia amemtaka mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga barabara ya Tanga - Pangani - Mkwaja - Bagamoyo (Makurunge) sehemu ya Tungamaa - Mkwaja – Mkange, kuilipa serikali fidia kutokana na uzembe uliofanya ujenzi usikamilike kwa wakati ilhali tayari serikali imetimiza upande wake wa mkataba ikiwamo kumlipa mkandarasi huyo.

Akizungumza kwa nyakati tofauti mkoani humo, Ulega alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya jitihada kubwa za ukarabati na ununuzi wa vivuko ili kurahisisha maisha ya wananchi na kwamba wananchi hawapaswi kupata shida wakati miundombinu ipo.

Kivuko aambacho kimeundiwa tume ni ya uchunguzi kinatoa huduma kati ya Pangani na Bweni na Ulega alisema lengo ni kuhakikisha kuwa kivuko hicho kinafanya kazi kwa wakati wote kama ilivyokusudiwa.

Naunda timu ya watu watatu, mmoja kutoka Ofisi ya Rais wa kutoka hapa na wawili Katibu Mkuu wa Ujenzi atawateua kutoka wizarani ili iniambie ni nini hasa kinaendelea hapa Pangani, haiwezi ikawa kila siku wananchi wanapata usumbufu”, amesisitiza Ulega.

Ulega amefanya maamuzi hayo kutokana na Kivuko hicho cha MV TANGA kushindwa kufanya kazi kwa siku nne huku watendaji na wasimamizi wakishindwa kufanya maamuzi ya haraka ya upatikanaji wa vipuri vya kufungwa katika kivuko hicho na kusisitiza kuwa endapo itabainika kuna hujuma zinafanyika katika kivuko hicho atachukua hatua za kinidhamu.

Akizungumza kabla ya Ulega, Mbunge wa Jimbo la Pangani ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alimuomba waziri huyo kushughulikia changamoto ya usafiri wa Kivuko cha MV TANGA ambacho ni muhimu na msaada kwa wananchi wa Pangani.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amekagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa.








Share To:

Post A Comment: