Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema kwamba  kuanzia  Mei 15, 2025 huduma mbalimbali zinazotolewa  na Wizara ya Madini zitaanza kutolewa rasmi katika jengo la Makao Makuu ya Wizara hiyo lililopo eneo la Mtumba, Mji wa Serikali kutokana na kukamilika kwa mradi wa jengo hilo.

Hayo yamebainishwa leo Mei 15, 2025 na Mhe. Mavunde wakati akizungumza na Menejimenti  ya Wizara, taasisi zake pamoja  na watumishi wa Wizara.

Waziri Mavunde ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Wizara kukamilisha jengo ambalo kwa sasa huduma zote zitatolewa hapo.

Akielezea kuhusu hali ilivyokuwa ,Waziri Mavunde ameeleza kuwa , awali huduma zilikuwa zinapatikana sehemu tofauti tofauti kutokana na ofisi kuwa mbalimbali lakini na kueleza kwamba sasa  huduma zitatolewa sehemu moja  na hivyo wadau kuondokana na usumbufu.

Awali, akiwakaribisha watumishi katika jengo jipya,  Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa ameishukuru Serikali  kwa kuweza kukamilisha ujenzi wa jengo na miundombinu mbalimbali itakayorahisisha utendajikazi na kutoa matokeo chanya kwa Sekta ya Madini kulingana na vipaumbele vyake.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini  Msafiri Mbibo amewapongeza watumishi wote wa Wizara kwa utendaji mzuri wa kazi katika mazingira yaliyokuwa yanawazunguka kwa kipindi chote cha  ujenzi wa makao makuu,  bila kujali changamoto zilikuwepo.

Aidha, kuhamia kwa Wizara katika Jengo jipya kunatimiza ahadi aliyoitoa Waziri Mavunde Kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi tarehe 20 Machi , 2025

Jengo hilo la Wizara limejengwa na Mkandarasi Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC) kwa gharama ya Shilingi bilioni 22.8 chini ya ushauri elekezi wa Wakala wa Majengo Tanzania ( TBA).

 Vision2030 : MadiniNiMaishaNaUtajiri






Share To:

Post A Comment: