Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) utakaofanyika Juni 19 mwaka huu. 

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa taarifa hiyo katika mkutano wa hadhara wilayani Sengerema mkoani Mwanza wakati akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa,  ambaye yuko ziarani mkoani Mwanza.

Waziri Ulega amewataka wananchi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo wa daraja hilo lenye  urefu wa kilometa 3 na barabara zake unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66 na linalotarajiwa kuwa refu kuliko yote katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. 

Ulega alisema kukamilika kwa daraja hilo ni mafanikio ya maono na jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mtangulizi wake, hayati John Magufuli. 

Namna pekee ya kuonyesha furaha yetu na shukrani zetu kwa mafanikio hayo ni kwenu wananchi wa Sengerema, mkoa wa Mwanza, Geita, mikoa yote ya kanda ya ziwa na wa Tanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi huo. Tunasema siku hiyo asiye mwana basi abebe jiwe.” alisema Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga. 

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo. 

"Jitayarisheni kwa wingi kumpokea kiongozi wetu mkuu atakapokuja kulifungua daraja hili Juni 19, 2025 ", alisema Waziri Mkuu. 

Ziara ya Waziri Mkuu mkoani Mwanza ni ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo Ulega alitumia mkutano wa Sengerema kumweleza Waziri Mkuu kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha huduma za usafiri na uchukuzi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ujumla.

“Watu waliokuwa wanasafiri kwa zaidi ya saa mbili watakwenda kusafiri kwa wastani wa dakika tatu hadi tano, Tunamshukuru Mhe Rais kwa maono na maelekezo yake”, amesisitiza Ulega.

Ameongeza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 700 zimetumika katika ujenzi wa daraja hilo linalounganisha mji wa Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria ambalo ni la tatu kwa ukubwa duniani.

Aidha, Waziri Ulega amewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Sengerema kuhusu ujenzi wa barabara Segerema - Nyehunge (km 54.5) na Kamanga - Sengerema (km 32) kwa kiwango cha lami Serikali ipo katika hatua za mwisho za kumkabidhi Mkandarasi kazi ya ujenzi huo.









Share To:

Post A Comment: