Mradi wa Uwezeshaji kupitia ujuzi nchini (ESP) umeendelea kuwanufaisha vijana, wanawake na wanaume katika vyuo vya maendeleo ya wananchi nchini (FDC) kupata ujuzi wa kutengeneza bidhaa mbalilbali kwa lengo la kuinua uchumi wao. 

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa mradi huo Jijini Arusha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahera amesema mradi huo umeunga mkono jitihada za serikali zinazolenga kila kijana kupata ujuzi wa elimu ya amali ili kukabiliana na ukosefu wa ajira nchini. 

Aidha ameongeza kuwa uwepo wa mradi huo unaotekelezwa katika vyuo vya maendeleo ya wananchi 12 kati ya 54 nchi nzima, umeleta matokeo chanya na kubadili mtazamo wa vijana wengi, sambamba na kuchangamkia fulsa zinazowazunguka katika maeneo yao. 

"Kipekee napongeza ushirikiano mkubwa wanaotuonyesha  serikali ya Canada  hapa nchini  kwa kuandaa kozi mbalimbali zinazoendana na mahitaji yetu,  uwezeshaji wa vifaaa vya kisasa vya kufundishia, Karakana na kutujengea (DayCares) hii yote ikilenga kuibua na kuinua uchumi wa vijana wengi hapa nchini", 

"Pia ikumbukwe kuwa mradi huu haujawaacha nyuma wasichana wenye watoto ambao walikatiza masomo au kukosa nafasi ya kusoma, mradi huu unawawezesha kusoma  wakati huo na watoto wao wakipata masomo kwa uangalizi maalumu hatua inayowapa amani na utulivu wasichana hao wakati wa masomo" amefafanua Dkt. Mahera. 

Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Maendeleo,  Ubalozi wa Canada Nchini Tanzania Carol Mundle amesema kozi hiyo ya muda mfupi inayotolewa katika vyuo 12  yamewapa vijana fulsa ya kupata ujuzi na kubadilisha mtazamo katika maisha yao. 

Amefafanua kuwa katika mkutano huo wanalenga kupitia upya mpango wa utekelezaji wa mradi wa ESP na kuona hatua gani zimepigwa katika utelekelezaji vilevile kuweka mkakati wa  muendelezo wa kozi hizo mpya. 

"Tunajivunia ushirikiano huu mkuu kati ya Serikali ya Canada na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknojia na kwa umoja wetu tunategemea kupata matokeo chanya" ameeleza Mundle. 

Katika namna hiyohiyo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Singida na 

Mwenyekiti wa Bodi ya chuo cha maendeleo ya wananchi Singida (FDC) Ester Chaula amebainisha kuwa, mradi umewajengea uwezo wasichana kujitegemea, kuzalisha mali kwa familia zao na wao wenyewe. 

"Nashukuru kwa ufadhili wa Serikali ya Canada kwa kushirikiana na taasisi za vyuo nchini humo (CICan), uliozinduliwa mwaka 2021 na kulenga  kutekelezwa hadi 2028, umeleta manufaa yakiwemo mafunzo kwa wakufunzi, mafunzo juu ya usawa wa kijinsia, ufadhili wa vifaa vya TEHAMA kama Kompyuta, projector, internet pamoja na ujenzi wa vituo  vya uangalizi na kujifunzia watoto (Dycare)"ameeleza Chaula. 

Vilevile mmoja wa wanufaika wa mafunzo ya Uwezeshaji kupitia Ujuzi (ESP) kutoka Mkoa wa Katavi Happy Matofali  (20)mama wa watoto( 2) amebainisha mafanikio yake baada ya kupata elimu ya mafunzo hayo ikiwemo ujuzi  wa kupika na namna ya kuwahudumia wateja kwa ukarimu. 

Amepongeza Mradi huo ambao umewakumbuka wasichana wenye watoto kupata ujuzi, hatua itakayoinua uchumi wa wanawake na wasichana wengi nchini ikiwemo kujitegemea na kujudumia familia zao. 

"Nina furaha sana kwa sababu ninapata masomo wakati huohuo na watoto wangu wakiwa wanapata elimu katika darasa lao, kwa hiyo sote kwa pamoja tunasoma, ninasoma kwa utulivu tofauti na kumuacha mtoto nyumbani, nimefanikiwa kupata ujuzi na maarifa yatakayonifaa baadaye, 

"Kwa sasa ninaweza kupika vyakula mbalimbali, hivyo ninaweza kujiajiri au kuajiriwa, qina cha kuwalipa hawa Wafadhili maana wamenitoa gizani" amesema Happy. 

Vyuo na  Taasisi za Ufundi Kanada (CICan) CICan ni sauti ya kitaifa na kimataifa ya vyuo na taasisi za elimu ya juu nchini Kanada, inayounganisha taasisi wanachama na washirika kutoka kote duniani, ikiwemo katika nchi zinazoendelea kwa lengo la kupunguza umasikini na ukosefu wa usawa, hasa kwa wanawake, vijana na makundi yaliyo katika mazingira magumu, kwa kubadilisha mifumo ya elimu ya juu na kutoa mafunzo yanayozingatia mahitaji ya soko la ajira.



























Share To:

Post A Comment: