Na Stanley Mwalongo- ZANZIBAR
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inashiriki maonesho ya Wiki ya Afya Zanzibar yaliyoanza jana Mei 4,na yatafikia tamati Mei 10, 2025 katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.
Akizungumza katika maonesho hayo leo Mei 5, 2025 Meneja Uhusiano wa MOI, Bw. Patrick Mvungi amesema lengo la kushiriki wiki hiyo ni kunadi huduma za kibingwa na kibobezi za MOI wananchi wa Zanzibar na mataifa jirani.
“Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe Balozi , Dkt. Mpoki Ulisubisya ametuelekeza tushiriki katika wiki ya afya Zanzibar ili kutoa elimu na ushauri wa matibabu ya kibingwa na kibobezi ya mifupa, ubongo, mgongo, mishipa ya fahamu na viungo saidizi kwa washiriki wa maonesho haya” amesema Mvungi
Pia, Mvungi amesema kupitia maonesho hayo wananadi huduma ya wagonjwa maalum na wakimataifa inayopatikana MOI ambayo huduma zake ni za viwango vya kimataifa na za haraka ambapo wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali hufika MOI kupata huduma.
Kwa upande wake, Daktari bingwa wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu Dkt. Zarina Shabhay amesema wamejipanga vizuri kuwahudumia wananchi wa Zanzibar na Comoro watakaotembelea banda la MOI katika maonesho hayo na wale watakaonekana wanahitaji uchunguzi zaidi watapewa rufaa ya kwenda kutibiwa MOI.
Post A Comment: