Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itazifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa na Chama cha Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) katika Mkutano wa 12 wa Kitaaluma wa chama hicho unaofanyika katika Ukumbi wa Ngurdoto Mkoani Arusha.
Mheshimiwa Rais amesema hayo alipowasalimu wanachama wa TAPSEA kwa njia ya simu wakati wa Mkutano huo ambao amewakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango. Amewasihi wanachama hao kufanya kazi kwa bidii ili kukuza uchumi hali itakayopelekea kuongezeka kwa maslahi yao.
Aidha Mheshimiwa Rais amewahimiza wanachama wa TAPSEA kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa kuhakikisha wanaendelea kujiandikisha na kurekebisha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Akifungua Mkutano huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewahimiza Waandishi Waendesha Ofisi kujiweka tayari ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia kwa kuendelea kujifunza na kuwa wabunifu zaidi kwa kuwa ustadi katika TEHAMA unakuwa ni sifa muhimu katika majukumu yao.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa waajiri kuandaa mafunzo kazini na mafunzo ya muda mfupi ili kuwawezesha Waandishi Waendesha Ofisi kuhuisha ujuzi wao katika teknolojia mpya za ofisi na zile zinazoibukia ikiwa ni pamoja na matumizi adili ya kompyuta na programu zake. Amevitaka vyuo vinavyotoa mafunzo kwa kada hiyo kujitahidi kutoa mafunzo na kuboresha mitaala ili kuendana na mabadiliko yanayojitokeza na kuwawezesha Waandishi Waendesha Ofisi kufanya kazi katika mazingira ya sasa na yajayo.
Pia amewasihi wanachama wote wa TAPSEA kufanya jitihada za kutafuta nafasi mbalimbali za kujiendeleza ili kujipatia maarifa mapya na mbinu bora zaidi za utendaji kazi.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka Waandishi Waendesha Ofisi kutambua jukumu muhimu walilonalo la kulinda maadili ya kitaaluma hususan kutunza siri za ofisi, kuwa mwaminifu na kulinda mwonekano wa ofisi. Amewahimiza kuzingatia utunzaji wa siri za Serikali na Taasisi nyingine. Amesema katika ulimwengu wa ushindani wa kibiashara, uvujishaji wa siri unaweza kudhoofisha taasisi na hata kuhatarisha usalama wa nchi.
Makamu wa Rais amewaelekeza waajiri wote nchini kuwapa Waandishi Waendesha Ofisi na kada nyingine fursa ya kushiriki mikutano ya kitaaluma na kuwawezesha kibajeti na kilojistiki.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Kada ya Waandishi Waendesha Ofisi ni muhimu katika utumishi wa umma na sekta binafsi kwa kuwa ndiyo inayohusika na kupanga na kuratibu mikutano na miadi kwa ajili ya viongozi. Pia amesema kada hiyo huandaa na kutunza kumbukumbu za ofisi, kuandaa na kuchakata taarifa za ofisi pamoja na kuratibu shughuli mbalimbali za ofisi. Amesema kupitia majukumu hayo, kada hiyo inatoa mchango mkubwa katika kuboresha utendaji kazi wa idara, taasisi za Serikali na sekta binafsi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema Serikali kupitia Wizara hiyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa Viongozi wa TAPSEA kwa kusimamia utendaji kazi wa wataalamu wa kada hiyo pamoja na kutatua kero na changamoto mbalimbali za kisera na kiutendaji ili kuwezesha utoaji wa huduma bora na yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman amesema moja ya chama cha kitaaluma kinachoimarisha zaidi Muungano ni Chama Cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) ambapo kimeendelea kuhakikisha ushiriki wa wanachama kutoka pande zote za Tanzania. Amewapongeza kwa kuendelea kufanya kazi kubwa katika Ofisi wanazohudumu ikiwemo kutunza siri za Serikali.
Awali akisoma risala kwa niaba ya Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania, Mwenyekiti wa Chama hicho Bi. Zuhura Songambele ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutenga bajeti na kuboresha mazingira pamoja na miundombinu ya Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Tabora. Pia wameiomba Serikali kuendelea kuimarisha upatikanaji wa vifaa muhimu vya kufundishia ili kukiwezesha chuo hicho kuendelea kutoa zao bora la watumishi wa Umma.
Bi. Zuhura ametoa wito kwa Serikali kuendelea kusisitiza Waajiri kutekeleza maagizo yanayotolewa na Viongozi kupitia nyaraka mbalimbali za kiutumishi ikiwemo utekelezaji wa Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa Kada ya Waandishi Waendesha Ofisi pamoja na changamoto ya baadhi ya waajiri kutowaruhusu Watumishi wa kada hiyo kuhudhuria mikutano ya kitaaluma.
Mkutano huo wa 12 wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) unaofanyika tarehe 12 -17 Mei 2025, unahudhuriwa na Watumishi takriban 5,000 kutoka Wizara, Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Mashirika ya Umma, Asasi za Kiraia na Makampuni Binafsi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Wanachama hao wameendelea kukutana kila mwaka ili kujifunza na kupeana uzoefu wa masuala mbalimbali yanayohusu kada yao kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia na matumizi ya mifumo ya TEHAMA inayokua kwa kasi.
Post A Comment: