Wananchi wa Kijiji cha Nsekwa, Kata ya Nsekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi wametoa pongezi zao kwa Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kutengeneza barabara za lami Kilomita 3.73 ili kuwezesha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kupata barabara za lami katika kijiji chao ambazo zimeweza kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.

Diwani wa Kata ya Nsekwa, Mhe. Elijius Malando alisema, barabara hizo zimewasaidia wafanyabiashara kufika kijijini kwao kununua asali, karanga na mahindi ambapo kwa niaba ya wananchi ameishukuru serikali kwa kujenga barabara inayoanzia makao makuu ya Wilaya kuja kijiji cha Nsekwa kwani imewasaidia wananchi kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.

“Wananchi wamefurahi wanasafirisha bidhaa zao kwa urahisi na biashara zimeongezeka watu wamefungua maduka, tunamshukuru Rais Samia kwa barabara za lami ambazo zimewakomboa wajawazito waliokuwa wanajifungulia njiani kwasasa wanafika hospitali ya wilaya kwa urahisi”, alisema Mhe. Malando.

Naye, Mkazi wa kijiji cha Nsekwa Bw. Deogratius Nicholaus alisema, hapo awali usafiri ulikuwa shida walikuwa wanatumia nauli ya pikipiki shilingi 10,000 lakini sasa nauli ni shilingi 5000, pia walikuwa wanatumia masaa mawili hadi matatu kufika mjini lakini sasa wanatumia dakika 45 kufika mjini.

“Tunaishukuru serikali kutupatia barabara sasa tunafanya biashara kwa urahisi, kabla ya lami kulikuwa na michanga mingi, kutoka kijijini kwenda Inyonga tulikuwa tunatumia masaa mengi kupeleka wagonjwa na kufuata huduma za kijamii lakini sasa tunapita kwa urahisi”, alisema.

Kwa upande wake, Bi. Anusiata Simon mkazi wa kijiji cha Nsekwa, ameishukuru serikali kwa kujenga barabara ambazo zimerahisisha usafiri wa kutoka kijijini kwenda Inyonga hadi Mpanda na amesema kwasasa wakiagiza bidhaa zinafika kwa wakati na wanafanya biashara hadi usiku kwa sababu ya taa za barabarani zilizowekwa ambazo zimeongeza usalama na kijiji kimependeza.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Paul Mabaya, ameishukuru serikali kwa kuwapatia fedha takribani Bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami Km 3.73 ambazo ni barabara ya Inyonga-Nsekwa Km 2, Mapili-Utene Km1 na Uzega-Kafulu Km 0.73 zilizopo Kijiji cha Nsekwa katika Halmashauri ya Mlele ambapo barabara ya Utene na Inyonga mradi umekamilika asilimia 100 upo katika kipindi cha matazamio cha mwaka mmoja.



 


Share To:

Post A Comment: