Na. Saidina Msangi, WF, Bagamoyo, Pwani.
Watumishi na wananchi wa wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, wameishukuru Serikali kwa kuwapa mafunzo ya elimu ya fedha yanayotolewa na Wizara ya Fedha kwa kuwa yamewafungua na kuwapa mwanga wa kujiandaa kustaafu wakiwa na uchumi imara.
Walitoa shukrani hizo kwa nyakati tofauti Mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, baada ya mafunzo ya siku mbili yaliyotolewa na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha ukihusisha watumishi katika ukumbi wa mikutano wa wilaya, na wananchi katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, (TaSUBa).
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Zuwena Ungele, alisema kuwa elimu ya fedha waliyoipata imewapa motisha ya kuanza kujiandaa na maisha ya kustaafu.
‘’Sisi ni mabalozi wa watumishi wa Serikali kwa ujumla sasa unapostaafu ukawa na maisha mabaya unaleta picha mbaya kuwa unaweza kuwa mtumishi wa Serikali unastaafu ukiwa umechoka kimaisha hivyo tujipange kulinda taswira ya Serikali kwa kujiandaa kustaafu tukiwa imara kiuchumi’’, alisema Bi. Ungele.
Alisisitiza kuwa watumishi ni wastaafu watarajiwa hivyo ni vema kuanza kuweka mpango na maandalizi ya kustaafu mapema ili wakati ukifika wawe na akiba ya kuwawezesha kuishi Maisha yenye hadhi.
Aidha, wameishukuru Wizara kwa elimu ya fedha na kutoa rai kuwa elimu hiyo itolewe mara kwa mara ili iwe chachu ya kuhamasisha watumishi na wananchi kwa ujumla kujenga utaratibu wa kujiandaa na maisha ya kustaafu.
Akizungumza wakati akitoa elimu kwa watumishi na wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya alisema kuwa Serikali inatekeleza programu ya utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa wanapata elimu ya fedha ya kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu fedha zao.
‘‘Ni lazima kuwa makini sana katika kupanga matumizi ya fedha, hakikisha unasimamia mapato na matumizi, matumizi yasizidi mapato, kila fedha unayopata tunza asilimia kumi tuwe na utaratibu wa kuweka akiba katika sehemu rasmi kwani akiba haiozi na kuhakikisha kuwa unapochukua mikopo taasisi hiyo imesajiliwa na ina leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania,’’ alisisitiza Bw. Kibakaya.
Post A Comment: