Tanzania inaendelea na kampeni maalum za kuchanja mbwa na paka kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa ifikapo Mwaka 2030 ili kufikia lengo la Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amebainisha hayo Jijini Arusha wakati wa maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani, katika Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Manyara.
Akizungumza kwenye moja ya vituo vya kutolea chanjo hiyo katika Shule ya Msingi Naurei iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Prof. Shemdoe ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanaendelea kuchanja mbwa ili kuondokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa kuwa kutibu ugonjwa huo ni ghali kuliko kuuzuia.
“Kuna kampeni inayoendelea isemayo ifikapo Mwaka 2030 tuwe tumeondokana na kichaa cha mbwa kwa kufanya hili ni sisi hapa na ili tuweze kuuzuia kinachotakiwa ni kutoa hizi chanjo.” Amesema Prof. Shemdoe.
Ametaka kuondolewa kwa vikwazo kuunganisha nguvu kwenye sekta mbalimbali kupambana na kichaa cha mbwa pamoja na kuondoa vikwazo ili kuunganisha wadau katika kudhibiti ugonjwa huo.
Aidha, amesisitiza kuondolewa vikwazo kwa kuratibu kampeni ya kudhibiti kichaa cha mbwa ambapo chanjo itafanyika maeneo mbalimbali nchini kwa kipindi cha wiki mbili ili kufikia mbwa wengi.
Pia, amebainisha kuwa lengo la maadhimisho hayo mwaka huu ambayo kitaifa yamefanyika Mkoani Mwanza yenye kauli mbiu “Ondoa Vizingiti Vikwamishavyo Mapambano Dhidi ya Kichaa cha Mbwa” ni kuongeza ufahamu kwa kusudi la kuhakikisha kuwa mahusiano kati ya binadamu na wanyama kama mbwa na paka, yanabaki kuwa salama.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Benezeth Lutege amesema maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani hufanyika kama kumbukumbu ya kifo cha Louis Pasteur mwanakemia na mwanamicrobiolojia mfaransa ambaye alitengeneza chanjo ya kwanza ya kichaa cha mbwa.
Dkt. Lutege amesema maadhimisho hayo ya kutoa chanjo ya kichaa cha mbwa yanaenda sambamba na kutoa elimu juu ya ufugaji wa mbwa ikiwemo namna ya kuwatunza na kuwahudumia pamoja na utoaji wa chanjo mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Jamii kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Mbwa wa Afrika ambalo linatoa chanjo bure ya kichaa cha mbwa katika Kanda ya Kaskazini Bw. Jens Fissenebert amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika kutokomeza ugonjwa huo.
Amesema shirika hilo ambalo limekuwa likilea mbwa na paka waliotelekezwa mitaani na ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya matibabu linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kutofuga mifugo hiyo endapo kama hawana uwezo ya kuihudumia ili kuiondolea adha ya kuzagaa mitaani.
Nao baadhi ya wananchi waliofikisha mbwa kupatiwa chanjo ya kichaa cha mbwa wameshukuru kupatiwa chanjo hiyo na kuahidi kutoa elimu kwa wafugaji wenzao kuzingatia afya ya mifugo yao ili kuondokana na ugonjwa huo hatari kwa jamii hususan kwa watoto ambao wamekuwa wakiathirika zaidi kwa kung’atwa na mbwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 60,000 hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani, ambapo hapa nchini kwa mujibu wa Wizara ya Afya inadariwa watu 1,500 hufariki kwa ugonjwa huu kila mwaka. Takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 50 ya watu wanaoathirika na ugonjwa huu ni watoto chini ya umri wa miaka 15.
Siku ya kichaa cha mbwa duniani huadhimishwa Tarehe 28 Mwezi Septemba kila mwaka ili kuongeza uelewa kuhusu kujikinga na kuzuia ugonjwa wa kichaa cha mbwa na kutafakari mbinu mbalimbali za kuutokomeza ugonjwa huo ambao unahatarisha afya ya binadamu na wanyama.
Post A Comment: