Msimamizi wa Uchaguzi wa serikali za Mitaa katika Halmashauri ya wilaya ya Makete Wiliam Makufwe ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo amesema ikitokea mgombea amepatikana mmoja atapigiwa kura ya ndio au Hapana na hakutakuwa na utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024.


Makufwe ametoa kauli hiyo Septemba 26,2024 wakati akitoa mwelekeo wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2024 mbele ya viongozi wa vyama vya siasa,Viongozi wa dini,wadau wa maendeleo katika halmashauri hiyo na kueleza kuwa utaratibu wa kupita bila kupingwa hautakuwepo na kwa viongozi walioko madarakani uongozi wao utakoma ifikapo Oktoba 25,2024 na kuanzia Oktoba 11 hadi Oktoba 20 mwaka huu zoezi litafanyika la kujiandikisha wapiga kura ili kupata orodha yao.

Katika uchaguzi huo amesema watendaji wa vijiji na kata ambao ni wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika maeneo yao hawataruhusiwa kuandikisha au kuandaa orodha ya wapiga kura na jukumu hilo watapewa wataalamu wengine na wapiga kura watatambuliwa kwa kujiandikisha katika vijiji vyao au kutambuliwa na wakazi katika eneo husika huku zoezi la fomu za uteuzi na kurejeshwa kwa wagombea litafanyika kuanzia Novemba 1 hadi Novemba 7 mwaka huu katika kila kijiji na ofisi ya mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo Iwawa.

Mdau wa maendeleo wilayani Makete Egnatio Mtawa Mkurugenzi wa SUMASESU na Green FM ameshauri kutoa wagombea bora na kuepukana na kadhia ya rushwa katika uchaguzi ili kupata wagombea wanaoweza kuleta maendeleo katika Halmahauri husika bila kusahau kuwepo kwa mkazo wa hamasa itakayosaidia wananchi kijitokeza kwa wingi kugombea nafasi na kuchagua viongozi

Naye Jasel Mwamwala Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Njombe ametaka vyombo vya habari kupewa nafasi katika mchakato huo sambamba na kuwepo kwa usawa kwa vyama shiriki ushauri ambao msimamizi wa uchaguzi amesema watauzingatia.

Caastory Ngonyani Afisa uchaguzi wilaya ya Makete ameviomba vyama vya siasa kushirikiana nao katika mchakato huo na kwa wale watakao kiuka kanuni na kujihusisha na vitendo vya rushwa hawatasita kuwaondoka katika zoezi hilo.
Share To:

Post A Comment: