Jeshi la Polisi mkoani Njombe limewakata watu watano wanaodhaniwa kuwa ni wezi wa bajaji iliyoibiwa mjini Makambako na Dereva kufungwa kamba na kutupwa katika kijiji cha Itipingi huku bajaji hiyo ikikutwa katika mtaa wa Kambarage mjini Njombe.

Mamia ya madereva bajaji na bodaboda mjini Njombe mapema asubuhi wamekusanyika katika Ofisi ya Mtaa wa Kambarage ambako wezi hao walikutwa huku wakishindwa kumuelewa kamanda wa Polisi na kutaka mkuu wa Mkoa afike na kutoa kauli.

Baada ya kuwasili mkuu wa mkoa Katika ofisi za Mtaa huo baadhi ya Madereva hao wamesema wamechoshwa na vitendo vya wenzao kutekwa,Kuporwa vyombo vya moto na wengine kuuawa kikatili na kutaka serikali iingilie kati.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kambarage mjini Njombe Francis Msanga amesema waliweka mtego baada ya kupata taarifa za bajaji kuwepo katika mtaa wake kwani mmiliki alifunga kifaa cha kubaini chombo kilipo yaani GPS na ndipo walipowakamata.

Aidha Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka baada ya kuwasili katika eneo hilo amewahakikishia madereva hao kuwa hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya wezi hao wanaorudisha nyuma jitihada za vijana katika kujitafutia riziki.

Mmiliki wa Bajaji hiyo Yenye namba MC 585 EHZ Bwana Ally Mohamed Makunga anayetajwa kuwa na Mwanajeshi anasema haikuwa kazi ngumu kubaini mali yake ilipo kutokana na teknolojia huku Mwenyekiti wa Madereva bajaji mkoa wa Njombe Richard Luganga akisema wamelazimika kumuomba mkuu wa mkoa afike kutokana na kuchoshwa na vitendo hivyo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amesema Jeshi lake liko imara katika kudhibiti matukio hayo hivyo anachoomba ni ushirikiano.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa madereva bajaji mkoani Njombe jumla ya bajaji 7 ziliibiwa katika kipindi cha mwaka mmoja  na sita kati yake zimepatikana huku hakuna hata mtuhumiwa aliyefungwa kwa kesi hizo.

Share To:

Post A Comment: