Na Imma Msumba: Tanga

MKURUGENZI mtendaji  wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Mhandisi Jumaa Hamsini ametoa wiki mbili  kwa Afisa biashara wa halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa anaongeza leseni za wafanyabiashara kutoka elfu nne zilizopo sasa na kufikia elfu kumi (10,000) ikiwa ni mpango mkakati  wa kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Mhandisi Hamsini ametoa magizo hayo leo Agosti 23,2024  wakati akizungumza na wakuu wa idara wa halmashauri hiyo katika kikao cha mipango kazi cha kwanza tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia mabadiliko aliyoyafanya hivi karibuni ambapo Mhandisi Hamsi amehamishiwa Jiji la Tanga  akitokea jijini Arusha.

"Afisa biashara nakuagiza biashara zote zilizopo kwenye jiji la Tanga mtu anayefanya biashara yeyote tujue jina lake biashara anayoifanya ana leseni au hana  na anafanya biashara gani ili leseni zetu zitoke kwenye elfu nne na ziende kwenye elfu kumi, wasiliana na Mamlaka ya mapato  tupate orodha ya wafanyabiashara wote waliopo ili tufanya tathimini ya wafanyabiashara wetu tulionao" alisisitiza Mhandisi Hamsini.

Aidha Mhandisi Hamsini amempa muda wa miezi sita afisa uchumi wa Jiji hilo kuhakikisha kuwa wanaongeza makusanyo ya fedha za ushuru 'Service Levy '  kutoka billioni nne zinazokusanywa kwa sasa hadi billioni kumi ili kuweza kutimiza malengo ya utoaji huduma kwa wananchi kupitia miradi mbalimbali wanayoitekeleza ikiwemo sekta ya elimu, Afya n.k.

"Afisa uchumi nakupa jukumu ndani ya miezi sita service Levy ipande kutoka shilingi billioni nne mpaka kufikia billion kumi mjue vyanzo vyenu vyote vya mapato na kuhakikisha vinakuwa ili kupandisha mapato katika halmashauri yetu". Amesema Hamsini.

"Maeneo ya mapato ya kwanza ni Ushuru wa mapato, ya pili ni leseni  ,Kodi ya majengo na  vingine ndio vinafuata  Afisa biashara nakupa wiki mbili biashara zote zilizopo kwenye jiji la Tanga anayefanya biashara yeyote  tujue jina lake ana leseni au hana na anafanya biashara gani ili leseni zetu zitoke kwenye elfu nne na ziende kwenye elfu 10 wasiliana  mamlaka ya mapato tupate orodha ya wafanyabiashara ili tupate usawa". Amesema Hamsini.

"Malengo ya kwanza Mimi huwa sipendi kupeleka fedha kidogo kidogo kwenye miradi  lazima tupeleke fedha za kutoaha kwenye miradi ili ikamilike kwa wakati lakini tuangalie ni yapi tumetekeleza na yapi hatujatekeleza , kabla sijaja Tanga tayari nilikuwa nimeshapata picha halisi ya Tanga sijaja na kipya nawategemea sana nyinyi wakuu wa idara tuweze kushirikiana". Amesisitiza Hamsini.

Aidha amewapongeza watumishi wa Jiji hilo kupitia wakuu wa idara  kwa kuendelea kusimamia na kutekeleza  kwa vitendo sekta ya uwekezaji ikiwemo uwepo wa jengo la kitega uchumi lililopo katika stendi kuu ya mabasi Kange  ambapo amewataka kuongeza kasi ili kuzidi kuipaisha Tanga kitaifa na kimataifa.

"Eneo lingine ni eneo la uwekezaji hongereni sana  nimetembelea pale Kange kwenye jengo la kitega uchumi lakini kwa kweli vile vyanzo hatuvitumii ipasavyo sasa niwa watake kila mmoja kwa taaluma yake tushauline kwa pamoja ili kuhakikisha lile eneo linakuwa sehemu ya mapato". Amesema Hamsini.

Ili kuhakikisha adhima ya Serikali inatimia katika kuendelea kutoka huduma bora kwa wananchi  mkurugenzi huyo amewataka watendaji na watumishi wote wa halmashauri hiyo kutoa ushirikiano kwa kila mmoja kupitia sekta mbalimbali sambamba na kuimarisha utendaji katika wao huku akimtaka Afisa utumishi kujali maslahi ya kila mmoja.












Share To:

Post A Comment: