Wafanyabiashara 112 wa mazao ambao waliingia ubia  na halmashauri ya mji wa Makambako katika ujenzi wa  soko la mazao kiumba lililopo kata ya Lyamkena wametakiwa kuhamia kwenye soko hilo huku halmashauri ikitakiwa kuzuia  magari yanayobeba mzigo kuanzia tani tatu kutoshusha wala kupakia mazao soko kuu.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka wakati akizungumza na wafanyabiashara hao katika ofisi za halmashauri ya mji wa Makambako,ambapo amewataka wafanyabiashara hao kuhamia katika soko hilo huku akitaka wafanyabiashara wa mazao wenye mitaji midogo kuendelea na biashara zao kwenye masoko waliyopo ikiwemo soko kuu, Maguvani na Magegele.

Agizo hili limetolewa ikiwa ni baada ya zoezi la awali la halmashauri ya mji wa Makambako la kutaka kuwahamishia wafanyabiashara wote wa mazao ambao wanafanyiabiashara zao kwenye maeneo yasiyo rasmi kuzuiwa na mkuu wa mkoa huyo disemba 18, 2023 akiwa katika mkutano wa hadhara na wananchi standi ya zamani mjini Makambako baada ya wajasiliamali wadogo kulalamikia zoezi hilo kwa madai ya kwamba nao watakiwa kuhamia kiumba licha ya kuwa na mitaji midogo.

Baadhi ya madiwani mjini Makambako, Diwani wa kata ya Mahongole Mario Kihombo na Diwani wa kata ya Lyamkena Salum Mlumbe wamesema maamuzi hayo ya mkuu wa mkoa yatakuwa na tija kwa halmashauri hasa katika kuongeza mapato.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Makambako Hanana Mfikwa amekubaliana na mpango huo na kueleza kuwa watasimamia maagizo hayo ili kuhakikisha yanatekelezwa huku akiwataka wafanyabiashara kulipokea zoezi hilo kwani lina nia njema.

Nao baadhi ya wafanyabiashara ambao wameingia mkataba wa ujenzi wa soko hilo na halmashauri akiwemo Mary Kyando, Abelnego Sanga na Ambwene Mbilinyi wamekubaliana na maagizo hayo huku wakikiri kupata hasara kubwa kabla ya maelekezo ya sasa kutolewa.

Soko la mazao la kiumba limejengwa kwa ubia kati ya halmashauri na wafanyabiashara ambapo halmashauri imewekeza zaidi ya milioni 300 kwa kulipa fidia ya maeneo hayo huku wafanyabiashara wakiwekeza zaidi ya bil.1 kwa kujenga  maghala na vizimba.

Share To:

Post A Comment: