Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kufanya filamu nyingine ya Royal Tour katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi baada ya kujionea wanyamapori mbalimbali katika Hifadhi hiyo.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo Julai 15, 2024 alipokuwa akizungumza na wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Mkoani Katavi.
Kauli hiyo inafuatia ombi la Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, la kuomba Royal Tour nyingine ifanyike mkoani humo.
“Nataka nikiri kwamba zile sifa alizozisema Waziri Mkuu Mstaafu kuhusu uwepo wa wanyama wengi na wa kuvutia katika Hifadhi ya Katavi nimeziona mwenyewe na zimetimia maana leo nilipita kwenye mbuga hiyo kuona ikoje mahitaji yakoje” amesema Rais Samia na kusisitiza:
“Tumeona mambo mengi ya kufanya mle ndani na suala la Royal Tour Waziri wa Maliasili na Utalii ameshaandika hivyo jipange na ukiwa tayari mimi mwenyewe nitakuja.
Rais Samia yupo katika ziara mkoani Katavi pamoja na mambo mengine kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo na leo ameingia Mkoani Rukwa.
Post A Comment: