Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Mhe. Zainab Katimba amewahakikishia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kichangachui iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji kuwa, katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali itaajiri walimu 12,000 ili kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu nchini.

Mhe. Katimba ameeleza mpango huo wa Serikali kuajiri walimu, mara baada ya kutakiwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango kujibu hoja ya upungufu wa walimu katika Shule ya Sekondari Kichangachui, iliyowasilishwa na mwanafunzi wa shule hiyo.

Mhe. Katimba ameanisha kuwa katika mwaka huu wa fedha, Serikali itaajiri walimu wapya 12,000 ili kuhakikisha shule zilizojengwa zinapata walimu watakaotoa elimu bora kwa watoto wa kitanzania kama ilivyokusudiwa. 

“Niwahakikishie wanafunzi kwamba, Serikali yenu makini inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua changamoto inayowakabili na ndio maana imepanga kuajiri walimu 12,000 ambao watapangwa katika shule mbalimbali nchini ikiwemo na shule yenu,” Mhe. Katimba amesisitiza.

Aidha, Mhe. Katimba amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kufanya tathmini ya upungufu wa walimu na kufanya msawazo wa walimu, ili kuziwezesha shule zenye upungufu mkubwa wa walimu kupata walimu walau wachache wakati Serikali ikiendelea kukamilisha mchakato wa kuajiri walimu 12,000 katika mwaka huu wa fedha.

Sanjari na hilo, Mhe. Katimba ametoa wito kwa wanafunzi wa shule hiyo ya Sekondari ya Kichangachui na wengineo, kuhakikisha wanasoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao za kushika nafasi mbalimbali za uongozi na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha na inaendelea kuboresha miundombinu ya elimumsingi nchini, lengo likiwa ni kuwawezesha watoto wa kitanzania kuwa na mazingira rafiki ya kupata elimu bora itakayokuwa na tija katika kuliletea taifa maendeleo.

Share To:

Post A Comment: