Na,Chedaiwe Msuya-Wizara ya Fedha-Kigoma.


Wananchi Mkoani Kigoma wametakiwa kujenga utamaduni wa kuwekeza fedha zao kwa kununua Hati Fungani mbalimbali zinazouzwa na Serikali ili iwe moja ya vyanzo vya kujiongezea vipato badala ya kuweka fedha zao katika mfumo usio rasmi.

Akizungumza na Timu ya watalaamu kutoka Wizara ya Fedha, Katibu Tawala Mkoa Kigoma, Bw. Hassan Abassi Kaigwa alisema kuwa uzoefu unaonyesha watu wengi wanaonunua Hati Fungani za Serikali hunufaika kwa kupata faida muda mfupi huku mtaji wao ukiendelea kuwepo na kutoa wito kwa wananchi wanaomiliki fedha kuchangamkia fursa hiyo.

“ katika Hati Fungani za serikali kwa mwaka unaweza kupata faida kati ya asilimia 12 hai 15 ambapo kwa mtu aliyenunua bondi za thaman ya shilingi million 200 anauwezo wa kupata zaidi ya shilingi milioni 24 kwa mwaka huku mtaji wake ukiwa palepale, mzunguko huu wa fedha sio jambo la kulipuuzia hivyo ni muhimu kila mwananchi achangamkie fursa hii adhimu” Alisisitiza Bw. Kaigwa.

Alisema kuwa sio lazima watu wote wawe wafanyabiashara bali wengine wanaweza kuwa wadau au wabia wa benki ama uwekezaji ili wanaojua kufanya biashara wafanye shughuli hiyo kwa kutumia fedha za wale wasiojua kufanya biashara wakaamua kuwekeza.

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa kutokana na umuhimu wa elimu ya fedha katika kuwakomboa wananchi katika umaskini, Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Raisbwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeamua kuweka mkazo wa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili waweze kunufaika.

Bw. Kibakaya alisema kuwa mpaka sasa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo kwa Wizara ya Fedha kutumia watalaam wake wazunguke nchi nzima kutoa elimu kwa wajasiriamali, wakulima na watumishi wa umma kuwajengea uwezo wa mambo muhimu ya kuzingatiwa kwenye elimu ya fedha ikiwemo umuhimu wa uwekezaji na namna ya kulinda mitaji 

“Ndio wakati muafaka sasa ambapo Serikali yetu imeona kupitia huu mtaala mpya wa elimu ya fedha ifundishwe kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu na Wizara imepokea maelekezo kupitia Mhe.Rais kuhakikisha tunapita katika mikoa yote kuwapatia elimu wananchi wote ambao hawakufanikiwa kuipata katika mfumo rasmi”

Bw. Kibayakaya amebainisha kuwa katika kutekeleza agizo la Rais tayari awamu ya kwanza imekwishafanyika na sasa ni awamu ya pili imeanzia mkoani Kigoma ambapo jumla ya Halmashauri nne zitafikiwa na mpango huo.

Timu ya Wataalam wa Wizara ya Fedha imeanza ziara ya kutoa mafunzo kwa wananchi kwa makundirika mbalimbali Mkoani Kigoma ili kuwajengea uwezo na kutambua fulsa za kuwekeza, kujiongezea kipato, kufanya uwekezaji na kujiwekea akiba.
Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: