Na Denis Chambi, Tanga.


WAKALA wa usajili wa Biashara na Leseni 'Brela' umewataka wafanyabiashara na wajasiriamali kote nchini  kuona umuhimu wa kusajili majina ya biashara zao ili yaweze kutambulika kisheria na sio kusubiri wakati wapatapo changamoto ambapo wengi wamekuwa wakikutana na vikwazo mbalimbali.

Kufuata sheria na vigezo vilivyowekwa katika kusajili biashara kumekuwa kukiwanufaisha wafanyabiashara  wengi  hapa nchini ambapo wamekuwa wakipata tenda kutoka Serikalini kupitia taasisi mbalimbali.

Akizungumza na vyombo vya habari Juni 3,2024 katika maonyesho ya 11 ya Biashara  na utalii yanayoendelea kufanyika mkoani Tanga  Afisa  sheria kutoka Wakala wa usajili wa Biashara na Leseni 'BRELA' Lupakisyo Mwambinga amebainisha kuwa imekuwa ni kawaida ya wafanyabiashara wengi  kukimbilia ofisi hizo mara tu wanapopata  changamoto jambo ambalo  limekuwa likiwakosesha fursa mbalimbali.

"Tumekuwa tukitoa elimu ili kuwaeleza wafanyabiashara umuhimu wa kusajili au kurasimisha biashara zao  kwa sababu wengi wamekuwa mpaka wakipata changamoto ndio anakimbilia BRELA hivyo ni vyema wafanyabiashara wakatumia ofisi zetu kuiasimisha biashara zao  lakini pia kupata Leseni inayostahili"

Ameongeza kuwa  ili kuwasaidia watanzania hususani wafanyabiashara wakiwemo wajasiriamali wadogo wadogo  BRELA imekuwa ikitoa elimu mbalimbali ya kuwaonyesha ni namna gani wanaweza kujijengea mazingira mazuri katika shughuli zao zinazowapatia kipato na hatimaye kuwa sehemu ya kuchangia maendeleo kwa Taifa.

Akifungua maonyesho hayo mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka Brela kuendelea kutoa semina na elimu mbalimbali kwa wajasiriamali, wabunifu na wafanyabiashara  juu ya umuhimu wa kusajili majina ya biashara na kampuni zao ambayo yataendana asili ya Taifa Hali ambayo itasaidia na kuitangaza  Tanzania kimataifa.

"Huko nchi za nje kuna makampuni na taasisi zimesajili majina kama yanayopatikana Tanzania kwahiyo ni  vizuri BRELA mkatusaidia   tuweze kusajili majina yetu nadhani tufanye semina pamoja ya wabunifu  wajasiriamali na wafanyabiashara  kuhusu majina ya 'geographical' tuyafanye yawe ya kwetu"

Aidha Dkt Batilda amewataka wawekezaji  waliowekeza katika viwanda mbalimbali vilivyopo mkoani Tanga ambavyo haviendelei na shughuli ya uzalishaji kufanya  uwezekano wa kuviendeleza ili viweze kuzalisha na kuurudisha mkoa huo katika hadhi yake ambapo unatajwa kama moja wapo ya mikoa ambayo ilikuwa na viwanda vingi hapa nchini.

"Wale walionunua viwanda hapa Tanga na kivitelekeza tutawaita tukae nao tuone mustakabali wa viwanda hivyo ni Nini lakini bia hata viwanda ambavyo vinaingia ubia na kuweka hisa katika viwanda vyetu tutataka navyo kujua mustakabali wao ni nini hatutaki kuona kiwanda chetu kinanunuliwa ili kiuliwe tunataka tuone kwamba uwekezaji Tanga unaimarika"

Dkt Burianiamewataka Shirika la kumhudumia viwanda vidogo mkoa wa Tanga  'SIDO' kuwa na ushirikiano na wafanyabiashara pamoja na wajasiriamali wadogo kuwapa elimu juu ya bidhaa wanazozalisha wazingatie ubora ili kuweza kuingia katika soko la kiushindani ndani na nje ya Tanzania.
"Sido tutataka muwe karibu Sana na halmashauri zetu, wajasiriamali na wajumbe wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ninyi ndio mtakaokwenda kufungua fursa za uzalishaji kuanzia ngazi ya kata tunataka Kila Kijiji kiwe kinazalisha angalau bidhaa moja wapo na kukiongezea thamani"

Kwa upande wake Rais wa Chemba ya biashara Tanzania 'TCCIA' Andrew Minja  amesema Tanzania imekuwa ni kinara wa maonyesho ya biashara na utalii  ndani na nje ya nchi  ambayo yamekuwa yakiitangaza nchi kimataifa na kufungua fursa za kibiashara , wawekezaji kuja kuwekeza sambamba na kuuza bidhaa mbalimbali zinazozalishwa ambazo zimekuwa na ushindani wa kimataifa.

"Sisi TCCIA tunaongoza kwa maonyesho ya ndani na nje ya nchi, tuna maonyesho yanayofanyika Kila mkoa kila mwaka ,Kuna maonyesho yanayofanyika mkoani Mwanza kimataifa sasa hivi yana miaka 18 , tuna maonyesho yanafanyika Kigoma  yanayoitwa Tanzania bussiness Forum ambayo yanaiuza Tanzania  kwenye nchi za Burundi Kongo na  Malawi na tunapeleka kazi za wafanyabiashara  na wazalishaji kwenye nchi mbalimbali kwahiyo hii ni kqzi tunaendelea kunifanya kwaajili ya kuzitangaza bidhaa zetu za ndani" alisema Minja.



Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani (Kulia) akipata  maelezo kutoka kwa afisa usajili kutoka Wakala wa usajili wa biashara na leseni Julieth Kiwelu wakati alipotembelea Banda lao katika maonyesho ya 11 ya  biashara na utalii yanayoendelea mkoani Tanga.



Share To:

JOEL MADUKA

Post A Comment: